KAMANDA wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Murilo, amesema ni ngumu kubaini ni lini uchunguzi utakamilika wa tukio la mauaji ya askari polisi watatu na mmoja wa kampuni binafsi ya ulinzi, yaliyotokea Agosti 25, mwaka huu katika makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kenyata, jijini Dar es Salaam.
Mauaji hayo yalitokea baada ya majibizano ya risasi kati ya mtu aliyefahamika kwa jina la Hamza Hassan Mohamed na Jeshi la Polisi, ambapo askari hao watatu na mlinzi huyo mmoja wa Kampuni ya Ulinzi ya SGA, walifariki dunia na Hamza naye akifariki kwa kupigwa risasi muda mfupi baada ya kuua askari hao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kamanda Murilo alibainisha si rahisi kwa sasa kueleza ni lini uchunguzi wa tukio hilo utakamilika.
Kamanda Muliro alisema kinachofanywa kwa sasa, kulingana na maelekezo ni upelelezi utakaokuja na majibu ya chanzo cha tukio.
Alipoulizwa kama wamewaachia ndugu wa Hamza au bado wanawashikilia, Kamanda Murilo hakueleza moja kwa moja hilo, zaidi ya kile alichokisema kuwa, katika upelelezi kuna kumshikilia au kumzuia mtu na kumkamata.
Alifafanua kwamba, kumshikilia au kumzuia mtu na kumkamata ni vitu tofauti, ingawa jamii haifahamu hilo na kuongeza:,
“Naweza kuamua kukushikilia kwa muda fulani ili nipate taarifa vitu ninavyovihitaji katika upelelezi, nikikamilisha nakuacha uende zako, hii ni kumshikilia au kumzuia mtu wengi hudhani mtu amekamatwa kumbe ni tofauti,” alisema.
Kamanda Muliro alisema jambo pekee analoeleza kwa sasa ni kwamba wanaendelea na uchunguzi na unafanyika kwa mujibu wa sheria, wakikamilisha watapeleka taarifa kwa vyombo vyenye mamlaka ya kisheria kupewa taarifa hizo.
Aliongeza kwamba, baada ya kuwasilisha taarifa hiyo kwa vyombo hivyo, vyenyewe ndivyo vitaamua kama vitangaze kwa umma ama la.
NYUMBANI KWA FAMILIA YA HAMZA
Hata hivyo, gazeti hili lilifika nyumbani kwa familia ya marehemu Hamza na kukutana na mmoja wa watu aliyejitambulisha kuwa ndugu yake (pasipo kutaja jina), na kueleza kuwa wote wameachiliwa na Jeshi la Polisi, kwa sharti la kutokusafiri kwenda nje ya Dar es Salaam na nje ya nchi.
Awali, akizungumza wakati wa hafla ya kuaga miili ya askari waliofariki Agosti 27, mwaka huu, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Simon Sirro, alisema tukio hilo ni funzo kwa askari hao, kuongeza umakini na kutomuamini yeyote. Alisisitiza vyombo vya ulinzi na usalama vitaendelea kufanya uchunguzi na kuja na jawabu la chanzo cha tukio na ushauri wa nini kifanyike.
Na JUMA ISSIHAKA