SERIKALI ya Uswisi imeahidi kuendelea kuimarisha ushirikiano na uhusiano wa muda mrefu baina ya Tanzania na nchi hiyo takribani miaka 40 katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.
Ushirikiano huo ni katika sekta ya Afya, elimu na kusaidia katika juhudi za Serikali katika mapambano ya kuondokana na umasikini na kuinua kipato cha wananchi.
Hayo yameelezwa Wilayani Chamwino mkoani Dodoma na balozi wa Uswisi nchini Tanzania, Didier Chassot, wakati walipofanya ziara maalum ya kutembelea wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Maendeleo ya Jamii (TASAF III), kuzungumza nao na kuona namna wanavyotekeleza miradi yao katika Kijiji cha Wilunze Wilayani Chamwino Jijini hapa.
Ziara hiyo ilikuja muda mfupu baada ya ujumbe huo kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan na kufanya mazungumzo ya pamoja ambapo walizungumzia mashirikiano ya nchi hizo.
Balozi huyo amesema Uswisi itaendelea na jitihada zake za kutoa misaada mbalimbali kwa Tanzania ili Kunusuru kaya Masikini na kusaidia Serikali katika utekelezaji wa miradi ya Maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF, Ladislaus Mwamanga, amesema katika awamu ya kwanza ya mpango wa Kunusuru kaya Masikini zaidi ya kaya 200,000 zimenufaika kubadilisha maisha yao na kuondokana na umasikini.
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo, Patricia Danzi, amewapongeza wanufaika hao kwa kutekeleza miradi ya TASAF huku akieleza kuwa wadau hao wapo kwa ajili ya kuwasaidia lakini jukumu kubwa lipo kwao ambapo wanapaswa kufanya jitihada katika kutekeleza miradi hiyo ya Maendeleo.
“Nimefarijika kuona namna mnavyotekeleza miradi ya TASAF, endelezeni juhudi hizo ili niweze kusonga mbele zaidi, Uswisi tunaahidi kuendelea kuwasaidia ili niweze kusonga mbele zaidi na zaidi,”amesema.
Awali baadhi ya wanufaika na walengwa walionufaika na fedha zinazotokewa na Mfuko huo wameeleza nnamna walivyonufaikanna fedha hizo ikiwemo kujikwamua kiuchumi na kuondokana na umasikini pamoja na kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula katika familia zao.
Na Happiness Mtweve, Dodoma