SERIKALI imetangaza matokeo ya dawa saba za tiba asili zilizofanyiwa utafiti wa kuweza kutibu ugonjwa wa Uviko- 19, iwapo zitatumiwa.
Pia, imesema wamefanya utafiti katika Hospitali 12 za serikali na binafsi na umethibitisha kuwa dawa asili zilizofanyiwa uchunguzi, hazina madhara kwa binadamu, hivyo wananchi wapuuze taarifa potofu dhidi ya dawa hizo.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Tiba kutoka katika Wizara hiyo, Dk. Vivian Wonanji, alisema kutokana na tafiti zilizofanywa wamebaini kuwa matokeo ya awali ya uchunguzi za tiba asili kwa dawa saba zina uwezo wa mapambano ya ugonjwa huo.
Alisema kutokana na majaribio hayo ya kitafiti kwa dawa hizo saba zimepitishwa na baraza ili kuhakiki usalama na ufanisi wa dawa kwa kuwa wamejiridhisha kuwa salama na sahihi katika mapambano ya Uviko-19.
“Utafiti umefanyika kwa hospitali 12 za serikali na binafsi kwa wagonjwa wa Uviko-19, kwa wagonjwa waliolazwa katika hospitali hizo kuweza kupata nafuu,” alisema.
Kwa mujibu wa Dk. Vivian uchaguzi wa kufanya utafiti katika hospitali hizo ulizingatia idadi ya wagonjwa waliopelekwa wenye dalili za maambukizi na kuthibitishwa kuwa na ugonjwa.
Alisema utafiti uliotumika ni wa uangalizi ambapo watafiti hawakuhusika kuwapa wagonjwa dawa za tiba asili, bali waliwafuatilia wale wanaotumia kutokana na imani zao.
”Lengo lilikuwa ni kuthibitisha usalama wa dawa hizo huku watafiti wakiwa wamegawanywa katika makundi, kundi la kwanza ni wale waliokuwa wakitumia dawa asili na matibabu ya hospitali na kundi la pili ni wale ambao hawatumii dawa asili,” alisema.
Aliongeza: “Utafiti ulianza Februari mwaka huu na matokeo ya awali yanaonyesha dawa hizi za tiba asili ni salama, kwa kupitia vipimo vya maabara vya figo, ini na kwenye damu hakuna athari zilizoonekana kwa wagonjwa wanaozitumia,” alisema.
Pia alisema maendeleo ya kiafya kwa makundi hayo yanaonyesha kuwa wagonjwa wa Uviko-19 walikuwa wakitumia mchanganyiko wa tiba asili na matibabu mengine maumivu na dalili za ugonjwa huo yalipungua kwa haraka.
Alieleza kuwa katika mwendelezo wa ushahidi wa kisayansi wizara inatarajia kufanya utafiti wa jaribio kwa ajili ya tiba kwa kutumia baadhi ya dawa hizo na kutafiti matumizi sahihi, kuziorodhesha na kuboresha kwa ajili ya miongozo ya nchi.
“Utafiti umefanyika kwa kushirikisha wataalamu kutoka katika hizo hospitali shiriki, Chuo cha SUA,UDSM na MUHAS na wizara inawasihi wananchi kutumia dawa za tiba asili na tiba mbadala ambazo zimesajiliwa, hususan zilizothibitishwa ni salama na kuendelea kuchukua hatua ya kujikinga na ugonjwa huo,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uratibu na Kukuza Utafiti kutoka NIMR, Dk. Paul Kazyoba, alizitaja dawa hizo ni zile za kujifusha zilizochanganywa ambapo wagonjwa walikuwa wakitumia kama mchanganyiko wa malimao, tangawizi, kitungu swaumu na majani mbalimbali, ambapo ni salama kwa asilimia 49.2, NIMRCAF kwa asilimia 39.5, COVIDOL asilimia 25.6.
Nyingine ni Planet asilimia 23.6, Bupiji asilimia 10.3, Uzima asilimia 8.7, Canvotanxa asilimia 2.6 na Bingwa asilimia 0.5.
Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala na NIMR ilifanya utafiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili,Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Hospitali ya Rufaa ya Kanda (KCMC), Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando, Benjamin Mkapa, Hospitali ya Rufaa Dodoma, Amana, Temeke na Mwananyamala.
NA MARIAM MZIWANDA