WATAALAMU nchini wamethibitisha kuwa watu wanaogua ugonjwa wa UTI mara kwa mara, wanaweza kuwa na tatizo la kuwapo kwa mawe kwenye figo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya mfumo wa mkojo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dk. Remigius Rugakingira, amesema zipo dalili kuwa wanaogua ugonjwa wa UTI mara kwa mara, wanaweza kuwa na tatizo la kuwapo kwa mawe kwenye figo.
Kutokana na hatua hiyo ameshauri watu wanaokutwa na UTI mara kwa mara, wafanye uchunguzi wa kina kwani wanaweza kuwa na mawe kwenye figo.
Amesema, kuna baadhi ya bakteria kwenye mfumo wa mkojo ambao wanafanya utengenezaji wa mawe kuwa mkubwa kwenye figo.
“Mtu anayetibiwa UTI mara kwa mara, anaweza kuwa na bakteria wengi, ambao wanatengeza mawe kwenye figo kwa hiyo, ni bora akafanyiwa uchunguzi wa kina” alisema Daktari.
Amefafanua kuwa, hospitali ya Benjamin Mkapa wanao uwezo wa kubaini mawe hayo kupitia teknolojia ya vipimo ikiwemo CT SCAN na Utrasound.
Dk. Remigius amesisitiza kuwa, pia wanaweza kutibu tatizo hilo pasipo upasuaji kwa kuwa wana mashine ya Shock Wave Lithotripsy (SWL).
“Mashine hiyo ijulikanayo kama SWL inayotumia teknolojia kuyeyusha au kuyaponda mawe na kuyatoa kwa njia ya mkojo pasipo madhara yoyote,”amesema.
NA MARIAM MZIWANDA