WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Ummy Mwalimu, ametangaza kuanza rasmi mfumo wa utozaji wa ushuru wa uegeshaji wa magari kwa njia za kielektroniki, ifikapo Desemba Mosi, Mwaka huu.
Hatua hiyo inakuja baada ya mfumo huo kufungwa Oktoba 9, mwaka huu kufuatia malalamiko yaliyotolewa na wananchi ya kutoridhishwa na utaratibu huo mpya.
Pia Waziri Ummy ametoa siku 21 kwa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARULA), kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kabla ya kuanza upya mfumo huo.
Akizungumza Dar es Salaam, amesema hatua ya kufunguliwa upya kuanza mfumo huo, imekuja baada ya kujiridhisha kushughulikiwa changamoto zote zilizolalamikiwa na wananchi juu ya mfumo huo.
“Mfumo mpya wa ukusanyaji wa ushuru wa magari kwa njia ya kielektroniki, umesaidia kuzuia upotevu wa mapato uliokuwa unajitokeza, hivyo haina budi kuendelea kuutumia baada ya changamoto zote kutatuliwa,”amesema.
Amesema tangu mfumo ulipoanza kutumika kwa siku walikuwa wakikusanya sh. milioni 40 tofauti na kabla ya kuanza kutumika ambapo walikusanya sh. milioni 25.
Ummy aliyataja maboresho ambayo wameyafanya ili kuondoa changamoto hizo kuwa ni mteja kupewa ankara inayoonyesha kiasi anachodaiwa na eneo alilopaki chombo cha usafiri.
“Kupunguza gharama za makato kutoka sh. 4500 kwa siku na sh. 500 kwa saa mpaka Tsh. 2500 kwa siku na Tsh. 500 kwa saa ambayo zitatumika katika Mkoa wa Dar es Salaam.
“Sh.1500 kwa siku na sh.500 kwa saa gharama za mikoa ya Mwanza na Arusha, pia sh. 1000 kwa siku na sh. 300 kwa saa Dodoma, Mbeya na Tanga, ” alisema.
Pia alisema kuanzia sasa madeni ya maegesho ya magari yatalipwa ndani ya siku 14 bila ya faini, akishindwa mhusika atalipa faini sh.1000 tofauti na ilivyokuwa awali ambapo ilikuwa sh.3000.
Waziri Ummy alisema mgawanyo wa makato hayo yametokana na uhitaji wa maegesho katika mikoa hiyo.
Akizungumzia changamoto ambazo zilisababishwa mfumo huo kusitishwa ni wateja kutopewa taarifa za madeni na ankara za sehemu walizoegesha magari.
“Kuzidishiwa gharama ya madeni yao, kutopewa ya malipo (contro number), majibu mabaya kutoka kwa mawakala wa ukatishaji tiketi
“Pia naiagiza TARURA kutenga asilimia 40 itakayo kuwa inatokana na mapato hayo iliingie katika halmashauri kwa ajili ya kuweka jiji katika hali ya usafi wa mifereji, barabara na ukarabati wa barabara pia,” alisema.
Alisema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuweka miji katika hali ya usafi.
Mkurugenzi wa TARURA, Injinia Victor Seff, alisema wamejipanga vyema kuhakikisha wanaondoa changamoto zote zilizojitokeza.
Meneja wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Injinia Geofrey Mkinga alisema wamejipanga vizuri kuanza upya kwa mfumo huo kama yalivyotolewa maagizo na Waziri Ummy.
Kuhusu kufuta madeni yaliyotengenezwa kipindi cha mfumo wa kielektroniki wa awali sh. milioni 811, Dar es Salaam sh.milioni 525, Iringa sh.milioni 60 na sh.milioni 89 kwa Dodoma na Singida, alisema ametoa maagizo kwa TARURA.
“Nimemuagiza Katibu kushirikiana na TARURA kufuata sheria na taratibu za kufuta madeni hayo, kutokana na changamoto zilizobainishwa katika mfumo huo.
Alisema vyombo vya usafiri vinavyo milikiwa na walemavu, serikali na balozi, vyombo vya usafiri vinavyoegeshwa maeneo ya nyumba za ibada wakati wa ibada, vyombo vinavyoegeshwa wakati wa sherehe za serikali, havitakiwi kutozwa ushuru.
Na SUPERIUS ERNEST