SERIKALI imesema soko la madini ya vito duniani kwa sasa limeyumba, baada ya kutokea kwa ugonjwa wa Uviko- 19.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Madini, Dk.Dotto Biteko, alipomtembelea mchimbaji wa madini ya vito aina ya Rhodorite katika Kijiji cha Ng’alo, Kata ya Lubeho, Wilaya ya Gairo, mkoani Morogoro, wakati wa ziara yake ya kutembelea wachimbaji wadogo.
“Sasa madini ya vito yamekuwa yakikosa soko, serikali inaendelea kutafuta soko ili kuondoa changamoto iliyopo na kuondoa migongano baina ya wachimbaji na wafanyakazi wao,”alisema
Alisema wanunuzi wakubwa wa madini hayo ni Wachina na Wathailand na wataanza kuwatangazia fursa hiyo waje wanunue ili kunufaisha pande zote mbili.
Waziri Dk. Biteko alisema uchimbaji wa madini kwa miaka mingi ulikuwa ukifanywa na wanaume kuliko wanawake na kwamba, tafiti zilizopo kwa sasa zinaonyesha kati ya watu 100, wanawake saba pekee ndio wachimbaji.
Alisema wanawake wengi wako kwenye kutoa huduma za kupika chakula, kuuza maji na soda, hivyo wanawake waliojitokeza, wanapaswa kuungwa mkono na kuwatafutia masoko.
“Kumkuta mwanamke anachimba kama alivyo mchimbaji Fatuma Hassan ni wachache, ila tunawahamasisha wajitokeze katika sekta hii,”alisema.
Dk. Biteko alisema Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa maelekezo kwa wizara hiyo kuhakikisha changamoto zilizopo kwa wachimbaji zinatatuliwa.
Kwa upande wake, mmiliki wa Mgodi huo wa Madini ya Rhodorite, Fatuma Hassan, alisema wana changamoto ya soko la madini, vitendea kazi, ukosefu wa mitaji, kugawana kwa asilimia baina ya mchimbaji na wafanyakazi pamoja na uzalishaji mdogo.
Alisema awali soko kuu lilikuwa kutoka nchini China na Thailand na tangu kuanza kwa uchimbaji Mei, mwaka jana, amekuwa akichimba na kuhifadhi bila kupata soko.
Naye, Ofisa Madini Mkazi, Mkoa wa Morogoro, Emmanuel Shija, alisema masoko yanaendana na mahitaji ya kila mwezi, hivyo kama mkoa, wanaendelea kuwasimamia na kutoa elimu kwa wachimbaji katika kutanua soko la madini.
NA LATIFA GANZEL, MOROGORO