UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT), Mkoa wa Dar es Salaam, umetoa maelekezo manne kwa watendaji wake ngazi za Wilaya, Kata, Matawi na Mashina, likiwemo la kuhakikisha wanahamasisha kikamilifu sensa ya watu na makazi.
Maelekezo mengine ni kuhakikisha wanaingiza wanachama wapya na kuhamasisha wanawake kushiriki kikamilifu katika kuwania nafasi katika Uchaguzi wa ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Pia, umewataka watendaji hao kumsaidia Mwenyekiti wa CCM Rais Samia Suluhu Hassan kuyaelezea masuala muhimu ya kimaendeleo anayofanya ili kumtia moyo.
Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa wa Dar es Salaam, Florance Masunga, alipokuwa akizungumza na watendaji wa umoja huo wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salam, leo.
Kuhusu uchaguzi wa ndani wa CCM, Florance amewasisitiza wanawake kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi kwani kufanya hivyo kutasaidia wanawake kushika nafasi muhimu za maamuzi.
“Jitokezeni kuwania nafasi ndani ya Chama. Simamisheni wagombea wazuri na sisi majina yao yakiletwa na tukabaini kuwa ni wazuri tutawapitisha,” amesema mwenyekiti huyo.
Amesisitiza pia watendaji hao hasa ngazi ya mashina na matawi, kuingiza wanachama wapya na kuwasajili kielektoroniki.
Ameeleza, wanachama ndiyo uhai wa Chama na suala la kuwasajili kwa njia ya kielektroniki ni muhimu kwani bila kufanya hivyo mwanachama anapoteza uhalali na hatoweza kuchagua au kugombea nafasi za uongozi.
“Ninawapongeza kwani katika usajili wa kielektroniki wa wanachama wa CCM mkoa wa Dar es Salam umekuwa wapili kwa makusanyo ya ada na wanachama.Tuendelee kuingiza wanachama wapya hasa mabinti ambao watakuwa ni hazina ya baadye,”ameeleza Florance.
Kuhusu Rais Samia, Mwenyekiti huyo wa UWT amesema , amekuwa mstari wa mbele kupambania maendeleo ya taifa hivyo wana CCM hasa wanawake wanao wajibu wa kumuunga mkono.
“Tushikamane na Rais Samia kwa kuyasemea yale anayoyafanya ili jamii ijue. Yapo mambo mengi ya kimaendeleo ambayo Rais na Mwenyekiti wetu Samia anayafanya. Tumtie moyo na tusimame naye,”amebainisha.
Awali , Mwenyekiti wa UWT wa Wilaya ya Kinondoni, Anna Hangaya “Mama Makete’, amesisitiza wanawake kushiriki kikamilifu katika sensa na makazi.
Na MWAANDISHI WETU