UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama Cha Mapinduzi, Wilaya ya Dodoma Mjini, wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan, kuwezesha ujenzi wa madarasa, ambayo yamesaidia kupunguza msongamano kwa wanafunzi shuleni.
Akizungumza jijini Dodoma, Katibu wa UWT, Wilaya ya Dodoma Mjini, Ndaeni Isanja, amesema Rais Samia aliwezesha kupatikana mkopo wenye riba nafuu wa sh. trilioni 1.3 ambazo zilielekezwa katika maeneo mbalimbali ikiwemo ujenzi wa madarasa.
Amebainisha katika kipindi kifupi alichokaa madarakani, Rais Samia amesukuma gurudumu la maendeleo likiwemo ujenzi wa madarasa, barabara na halmashauri zimeendelea kukusanya mapato kwa kiwango bora.
“Rais Samia alifikiria kwa mapana sana, kwa sababu hakuzipeleka fedha hizo kuboresha huduma ya afya pekee, aliamua zielekezwe pia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ili watoto wapate elimu ambapo yamesaidia kupunguza msongamano wa watoto shuleni,” amesema.
Ndaeni amewataka wanawake kuendelea kumuunga mkono Rais Samia ili aendelee kuliongoza taifa kwa amani na mshikamano.
Katika hatua nyingine, amewahamasisha wanawake kujitokeza kwa wingi kuwania nafasi za uongozi ndani ya Chama na serikali kwa kuwa utafiti umeonyesha wanaopata nafasi ya uongozi wanafanya vizuri katika maeneo yao ya kazi.
Kuhusu uteuzi wa nafasi ya mgombea Uspika, Ndaeni amesema UWT inampongeza Dk. Tulia Ackson kwa kuaminiwa ndani ya Chama kuteuliwa kuwania nafasi hiyo kutokana na uzoefu, uadilifu na nafasi yake katika Bunge.
“Mchakato uliofanyika wa kumpata mgombea Uspika ndani ya Chama ulikuwa wa kidemokrasia kwa sababu kila mtu alikuwa na uhuru wa kuchukua fomu na watu wengi walionyesha mwitikio. Kamati mbalimbali za Chama zilikaa hadi mwisho na Kamati Kuu ilipokaa na kuamua kupitisha jina la Dk. Tulia kuwa ndiye anafaa,” alisema.
Na FRED ALFRED, DODOMA