UMOJA wa Wanawake Tanzania (UWT) wa Chama cha Mapinduzi, Mkoa wa Njombe, umeshika nafasi ya tatu katika usimamizi wa miradi ya kiuchumi ya Chama.
Umoja huo umeahidi kuongeza kasi hiyo kwa ajili ya matokeo bora zaidi.
Mwenyekiti wa UWT, Mkoa wa Njombe, Scholastika Kevela, aliahidi hayo muda mfupi, baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, kuwakabidhiwa cheti cha pongezi kutokana na ushindi huo, wakati wa kikao cha kawaida cha Baraza Kuu la UWT Taifa kilichofanyika Jijini Dodoma,
“Sisi kama wanawake wa UWT wa Njombe tumefarijika na ushindi huu, umetupa chachu ya kuendelea kuhakikisha tunaongeza usimamizi wa miradi hiyo kwa matokeo chanya ndani ya Chama,” alisisitiza.
Aliyataja malengo ya Umoja huo ni kuendelea kushirikiana pamoja na kuweka mkazo katika usimamizi wa miradi hiyo na mingine ya kimaendeleo inayotekelezwa na Chama kama moja ya majukumu yake.
Aliweka bayana kwamba usimamizi mzuri katika miradi hiyo, ndiyo njia pekee itakayokiwezesha Chama kupiga hatua mbalimbali za maendeleo kutokana na umuhimu wake katika kuchangia mapato ya Chama.
Nafasi ya kwanza katika eneo la usimamizi wa miradi hiyo ilichukuliwa na Mkoa wa Arusha huku Mkoa wa Mwanza ukichukia nafasi ya pili, ambapo mikoa hiyo yote ilikabidhiwa cheti cha pongezi kwa hatua hiyo.
UWT Mkoa wa Njombe, pia imeushukuru uongozi wa UWT Taifa kwa kutambua juhudi wanazozifanya na kutambua mchango wao huku ikiahidi kuendelea kutoa ushirikiano wa kutosha katika kukikuza Chama.
Katika hatua nyingine, Scholastika alipongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan kwa kulitumikia taifa.
“Tupo naye na tutaaendelea kumuunga mkono kwa vitendo katika harakati zake za ujenzi wa taifa, tukizidi kusisitiza kuwa kazi iendelee kama anavyosisitiza,” aliahidi.
NA MWANDISHI WETU, DODOMA