WAKALA wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Singida, unatarajia kutumia zaidi ya sh. bilioni 2.4, kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali 22 katika vijiji 14.
Meneja RUWASA Wilaya ya Singida Injinia Athumani Mkalimoto, aliyasema hayo, wakati akitoa taarifa mbele ya kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida.
Alisema taarifa hiyo ni ya utekelezaji wa shughuli za serikali katika robo ya kwanza iliyoanza Julai hadi Septemba, mwaka huu.
Mlimoto alisema miradi mipya inatarajiwa kujengwa katika vijiji vya Ughandi B, Mitula, Migugu na Mwighanji.
“Usanifu na uchimbaji unafanyika katika Kijiji cha Ntondo, Kinyamwenda, Msikii, Sekoture, Lamba, Mkenge, Makuro, Misinko na Makhandi. Tutaendelea kutatua changamoto kwa kukarabati miradi ya maji katika Vijiji vya Matumbo, Kinyagigi na Ghata-Mwachambia, miardi hii itakamilika kabla ya Desemba mwaka huu,”alisema meneja huyo.
Katika hatua nyingine, Injinia huyo alitaja miradi ambayo ipo tayari kuanza kujengewa miundombinu ya maji baada ya kupokea fedha za P4R awamu ya pili, ni katika vijiji vya Mitula, Ghandi B, Migugu na Mwighanji. Mradi wa Ughandi B umeanza kutekelezwa.
“Baada ya kukamilisha miradi yote iliyoainishwa, wananchi 37,500 watapata huduma ya maji safi na salama na yenye kutosheleza.Na hivyo kufanya asilimia ya huduma kuongezeka kutoka asilimia 67.4 kwa sasa hadi 76. Ifikapo mwaka 2025, RUWASA Wilaya ya Singida ina malengo ya kuhakikisha asilimia 85 ya wananchi wanaopata maji safi na salama na yenye kutosheleza”,alisema Mkalimoto.
Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskasi Muragili, alisema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, imetoa mabilioni kwa mkoa wa Singida kwa ajili ya miradi mbalimbali ikiwemo ya barabara.
“Kilichopo mbele yetu wakazi wa Mkoa wa Singida tukiwemo sisi wa Wilaya ya Singida ni kushiriki kikamilifu katika kuchapakazi za miradi mbalimbali ya maendeleo. Hiyo ni shukrani pekee na pongezi kwa Rais wetu,”alisema.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Elia Digha, aliwataka madiwani na wananchi wa wilaya hiyo kutoa ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambayo bado ni changamoto bila kujali itikadi za vyama vya siasa.
Na Nathaniel Limu, Singida