NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja, amewataka viongozi wa Kanda ya Ziwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na changamoto za uhifadhi wa mazingira, hususan katika mikoa wa Mwanza na Simiyu, lengo likiwa ni kuboresha maisha ya kila kiumbe ya sasa na baadaye.
Rai hiyo ameitoa baada ya kupokea taarifa ya hali ya uhifadhi mkoani Mwanza, ambapo amezitaka jamii za wakulima na wafugaji zinazoishi maeneo ya hifadhi za misitu ziishi kwa amani na kuhifadhi mazingira kwa faida ya sasa na vizazi vijavyo.
Ametaja miongoni mwa changamoto zinazowakabili wananchi wa vijiji vinavyouzunguka msitu nchini ni elimu ya uhifadhi na athari zake, namna wanavyoweza kutumia hifadhi za misitu kutokomeza umasikini pamoja na kutokuwepo na matumizi bora ya ardhi.
Kutokana na hali hiyo, naibu waziri huyo alitoa rai kwa uongozi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), viongozi wa wilaya na vijiji kushirikiana pamoja kuelimisha wananchi wanaozunguka hifadhi za misitu, huku wakala ukitakiwa kutafuta miradi kupitia programu za kurudisha kwa jamii (CSR) kusaidia jamii kando mwa misitu.
“Ninafahamu kuwa kuna Kamati ya Mawaziri wanane iliyoundwa kushughulikia migogoro ya mipaka katika hifadhi za misitu, lakini wakati tukisubiri kamati hiyo kutoa mapendekezo yake, tuanze sasa kutoa elimu na kuwafanyia vitu vingi vya CSR ikiwemo kuwapelekea miradi ya Ufugaji Nyuki pamoja na Kilimo na Ufugaji bora ili watuelewe, na wajue tunapohimiza uhifadhi tuna lengo zuri,” amesema.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, amesema misitu iliyopo Kanda ya Ziwa haina hali nzuri na kuwataka viongozi kuchukua hatua za kuhimiza uhifadhi.
“Msitu yetu tumeiona katika ramani kubwa ya Kanda ya Ziwa, niwaombe viongozi tuwe na moyo wa kihifadhi, kanda hii kuna maeneo yalikuwa na mvua mara mbili kwa mwaka na sasa mvua ni za kubahatisha huku maeneo mengine yakikumbwa na ukame, hakuna muujiza ni uhifadhi. Kuna maeneo yalikuwa na mito mikubwa sasa imekauka na ng’ombe wamekufa, tuna haja kubwa ya kuwekeza kwenye mabadiliko ya tabia nchi,” amesema.
Aliongeza kuwa: “Viongozi wote kwa pamoja tuwe na wimbo mmoja, wabunge, viongozi wa serikali kuu, taasisi za umma na binafsi tushirikiane sote kwa pamoja kuhifadhi misitu yetu kwa faida ya kizazi kijacho ambacho tusipofanya maamuzi magumu leo hii hakitakuwa na furaha, tusiwe wabinafsi.”
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salum Kali, Mkuu wa Wilaya ya Busega, Gabriel Zakaria na wabunge wawakilishi wa wananchi wanaoishi kando mwa hifadhi za misitu, walisema uhifadhi nchini una faida kubwa, muhimu ni kuwepo na programu ya kutoa mafuzo ya uhifadhi sambamba na kuanzisha miradi yenye manufaa katika uhifadhi wa misitu na kuleta manufaa kwa wananchi.
Awali, Kamishna wa Uhifadhi wa TFS, Profesa Dos Santos Silayo, amesema wakala uko tayari kushirikiana na viongozi wa Kanda ya Ziwa katika kuhakikisha uhifadhi unafanikiwa.
Amesisitiza kuwa pamoja na changamoto mbalimbali za uhifadhi nchini, wakala utaendelea kuhakikisha kunakuwa na usimamizi endelevu wa rasilimali za misitu na nyuki ili kuchangia kikamilifu mahitaji ya kijamii, kiuchumi, kiikolojia na kiutamaduni kwa kizazi cha sasa na kijacho.