VIONGOZI wanaotekeleza Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) wamerudhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya walengwa kupitia mradi wa nguvu kazi hususani kwenye kilimo cha Korosho na Zabibu Vijiji vya Handali na Mlowa Chamwino mkoani Dodoma, ambapo kupitia shamba darasa la vikundi walengwa wameweza kuanzisha miradi binafsi.
Pia TASAF imewapongeza wataalam ambao ni maofisa ugani kwa kufanya kazi yao kwa kujituma, uadilifu na weledi ambayo ndio imekuwa siri ya mafanikio ya walengwa wa katika utekelezaji wa miradi ya kilimo baada ya kuwapatia elimu na kuwatembelea kwa ukaguzi, maendeleo ya shamba na kuwashauri.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TASAF Zuhura Mdungi ametoa kauli hiyo jijini humo wakati wa ziara iliyofanywa na viongozi na watendaji wa TASAF kwa ajili ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na walengwa, inayofadhiliwa kupitia mpango huo katika Wilaya ya Chamwino vijiji vya Handali na Mlowa mkoani hapa.
Akizungumza wakati wa ziara ya kikazi ya kutembelea miradi hiyo ya TASAF yenye lengo la kutoa ajira za muda kwa walengwa wa mpango, amesema miradi hiyo imesaidia kutoa elimu kwa walengwa iliopelekea kuanzisha mashamba yao wenyewe ili kujiinua kiuchumi.
Pia kupitia miradi hiyo imesaidia asilimia 80 ya walengwa wa mpango huo kuweza kujiajiri wao baada kupata elimu kutoka kwa maafisa Ugani ya kuendesha kilimo cha mazao hayo.
Zuhura amesema miradi ya nguvu kazi imeleta matokeo chanya kwa walengwa wa mpango huo, kwasababu wengi wamejikwamua kiuchumi kwa kujipatia kipato kutokana na ajira za muda katika mashamba madarasa yanayosimamiwa na viongozi wa serikali ya kijiji pamoja na waratibu wa mpango wa kunusuru Kaya maskini katika eneo husika.
Mkuu huyo ameishukuru na kuipongeza serikali ya vijijini hivyo kwa kuweka mipango mizuri na kuwasimamia kwa karibu walengwa wa TASAF katika kuhakikisha maofisa ugani wanatoa elimu ipasavyo na walengwa wanapoke na kutekeleza.
“Tumeshuhudia walengwa walivyotekeleza miradi ya kilimo cha Zabibu na Korosho kupitia mashamba darasa na baadaye mashamba binafsi, tumeona ustawi wa miradi kwa kweli tumeridhishw na wao wmetuhakikishia kuwa soko liko vizuri na watafanikiwa kupata kupao kitakachowawezesha kuongeza uchumi na kujikwamua na umasikini.” amesema Zuhura.
Mkuu wa huyo wa kitengo cha mawasiliano amebainisha kuwa miradi hiyo imesaidia walengwa wengi kutoka katika vikundi vya pamoja na kwenda kuanzisha mashamba yao wenyewe.
Aidha, amewataka maafisa ugani kuendelea kuwapa elimu walengwa hao ili waweze kufanikisha kilimo cha Korosho na Zabibu ambacho ni cha muda mrefu na huleta tija kwa wakulima.
Awali akizungumza na waandishi wa Habari Mlengwa wa TASAF na msimamizi wa shamba la Korosho Kijiji cha Mlowa, Yohana Malecela amesema kilimo cha Korosho ni kizuri kwao kwa sababu ni zao la biashara tofauti na mazao mengine wanayolima.
“Sisi walengwa tunashukuru sana TASAF kutokana na kuanzisha mradi huo,kwa sababu umesaidia walengwa wengi kujikwamua kiuchumia,”amesema Malecela.
Kwa upande wake Ofisa Kilimo wa Kata ya Mlowa Winnie Ndahani ameeleza kuwa, wao kama wataalamu wa Kilimo wamekuwa wakishirikiana na wakulima ambao ni walengwa ili kuhakikisha kilimo cha Korosho kinasonga mbele.
Amesema wakulima wa kijiji cha Mlowa wameonyesha kuvutiwa na Kilimo cha Korosho kutokana na kudai kina faida kubwa na hudumu kwa muda mrefu tofauti na mazao mengine.
Na Happiness Mtweve,Dodoma