KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Burundi, hususan katika masuala ya kiuchumi utaendelea kuimarika kwa maslahi ya wananchi.
Amesema ushirikiano huo katika masuala ya kisiasa baina ya Chama cha CNDD-FDD na CCM,umetajwa kuwa ni kiungo muhimu kwa viongozi wa nchi hizo, kwa pamoja wamekuwa wakishirikiana katika utendaji wa Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere iliyopo Kibaha mkoani Pwani.
Chongolo alisema hayo jijini Dar es Salaam, baada ya kumpokea Katibu Mkuu wa Chama cha CNDD-FDD, Reverien Ndikuriyo, aliyewasili nchini kwa ziara ya siku tatu.
Katibu Mkuu Chongolo alisema ushirikiano baina ya nchi hizo umeendelea kuimarika, ambapo serikali zake zimeendelea kushirikiana katika fursa za kiuchumi ikiwemo katika uwekezaji wa kiwanda cha mbolea kinachojengwa Dodoma.
“Hivi karibuni nilitembelea kiwanda hicho ambacho kina tija kubwa kwa nchi mbili hizo,ni uwekezaji mkubwa wa zaidi ya sh. bilioni 440,” alisema.
Alisema ushirikiano katika uwekezaji sekta ya nishati hususan katika mradi mkubwa wa umeme wa Rusumo, ambao utekelezaji wake upo katika hatua za mwisho, ni wa kuigwa ambao unadhihirisha umoja kwa nchi za Afrika katika maendeleo.
Chongolo aliongeza kwamba, ushirikiano huo unajengwa na uhusiano mzuri wa serikali za nchi hizo, ambapo ujenzi wa reli unaoendelea ukiunganisha Tanzania na Burundi katika kusaidia mawasiliano na biashara ni kielelezo cha kuendeleza historia zilizopo.
“Kubwa zaidi ni katika ushirikiano sekta ya elimu,ambapo vyama vyetu kwa pamoja tumehakikisha Shule ya Uongozi ambayo kwa sasa Mkuu wake ameteuliwa ambaye ni Profesa Mwandamizi Mercelina Chijoriga, tunashirikiana ipasavyo,” alisema.
Alisema katika ziara hiyo, Katibu Mkuu wa Chama cha CNDD-FDD , Ndikuriyo leo anatarajiwa kutembelea Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere Kibaha ambayo imejengwa kwa ushirikiano wa vyama vya nchi sita za ukombozi Kusini mwa Afrika ambazo ni CCM,SWAPO,FRELINO, ANC ya Afrika Kusini na MPLA ya Angola na ZANU PF.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama cha CNDD-FDD, Ndikuriyo, alipongeza uhusiano mzuri uliopo kati ya Tanzania na Burundi na kueleza kwamba kwa sasa nchi yake imeamua kuandaa viongozi ambao watakuwa na weledi katika siasa.
Alisema matarajio ni kutumia shule hiyo kupanua wigo wa elimu ya uongozi, kwa kuwa wamekuwa wakipeleka viongozi wengi nje ya nchi bila kuwa na mafanikio ambao wengi hawarudi kuitumikia nchi yao.
“Tanzania ni nchi muhimu kwa Burundi kwa kuwa ushirikiano katika siasa na usafirishaji wa bidhaa umekuwa ukisaidia kukuza uchumi, tunapenda kuwakaribisha katika kubadilishana uzoefu wa sekta ya michezo nafuatilia sana mpira wa Tanzania kwa kuwa mna wachezaji wengi kutoka nchini kwetu.
“Pia, nawaalika viongozi wa CCM katika uzinduzi wa uwanja wetu wa kisasa ambao upo karibu kabisa na Kigoma,” alisema.
NA MARIAM MZIWANDA