KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo, amezindua barabara ya Ukombozi inayokwenda Shule ya Uongozi ya Mwalimu Nyerere, Kibaha mkoani Pwani na kuungwa mkono na vyama vitano rafiki vilivyopigania ukombozi wa Afrika.
Aidha, amesema vyama vya upinzani vitasubiri kwa zaidi ya miaka 100 kuona CCM inatoka madarakani kwa kuwa imejidhatiti kuendelea kuongoza nchi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi barabara hiyo yenye urefu wa kilomita mbili, kwenda katika chuo hicho cha kwanza Afrika kwa ukubwa, Chongolo alisema CCM itaendelea kuwa Chama bora na kilichojidhatiti kuongoza nchi.
“Wasubiri baada ya miaka 100 labda ndio waongoze nchi, wapo wanaojiuliza na kusemasema huko, kwa nini barabara hii inakuja kuzinduliwa na Katibu Mkuu wa CCM, kwani serikali ni ya nani na hayo yanayofanywa inatekelezwa Ilani, wajue serikali yetu Chama chetu na miundombinu hii ni ya kwetu,” alisema.
Katibu Mkuu Chongolo alitumia fursa hiyo, kuwataka wananchi wa Kibaha kutumia shule hiyo na miundombinu ya barabara ipasavyo, kwa maendeleo ya uchumi na kufungua milango ya maendeleo.
“Wananchi wa Kibaha, Pwani tumieni miundombinu hii ya Chuo cha Uongozi Cha Mwalimu Nyerere kujikomboa kiuchumi kwa kuhakikisha fursa za miundombinu zinawaletea maendeleo,” alisema.
Aidha, alikemea uharibifu wa miundombinu ya barabara na kuelekeza barabara ya Ukombozi, ilindwe na kuwekewa mazingira ya kudumu kwa maslahi ya vizazi vijavyo.
“Sisi tumekuja kufungua njia, tunatambua ukombozi tulishakamilisha, tuna historia, tunahitaji ukombozi unaoenda pamoja na uchumi katika mataifa yetu, wito wangu kwa wana Kibaha tumeleta chuo ni lazima kiwanufaishe kiuchumi,” alisema.
Alisema chuo hicho kimejengwa kwa ushirikiano na vyama vya CCM, ZANU PF (Zimbabwe), FRELIMO (Msumbiji), ANC (Afrika Kusini), MPLA (Angola) na SWAPO (Namibia).
Wakishuhudia uzinduzi huo, Makatibu wakuu wa vyama rafiki washirika akiwemo wa ZANU PF, MPLA, SWAPO, FRELIMO na ANC, Katibu wa Chama Cha SWAPO, Sophia Shinengwa, alisema alama aliyoacha aliyekuwa Rais Dk. John Magufuli ya kuimarisha mahusiano yaliyopo katika vyama sita washirika wa ukombozi ni muhimu kuendelezwa.
Sophia alifafanua, Jina la Mwalimu Julius Nyerere limetumika katika chuo hicho ili kulinda fikra alizozianzisha za kulikomboa Bara la Afrika, ili zitekelezwa kwa vitendo kwa sababu katika chuo hicho watapatikana viongozi ambao watakuwa na uzalendo wa hali ya juu.
“Viongozi hao watapatiwa mafunzo yatayoakisi Itikadi na falsafa za Mwalimu Nyerere,” alisema.
Mwakilishi kutoka ANC, Sibongile Desani alisema Tanzania ni nchi ya kuigwa na uzinduzi wa barabara hiyo unaunganisha uhusiano wa kihistoria.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa ZANU PF, Dk. Obeid Mpofu alisema hatua ya vyama hivyo rafiki vya Kusini mwa Afrika kujenga chuo hicho, ni kuenzi harakati za waasisi wa mataifa hayo katika kumuenzi Mwalimu Nyerere.
Mpofu, alisema kuwa Tanzania ilikuwa muhimili wa Mapinduzi kwa nchi za Kusini mwa Afrika na kuenzi mawazo yake.
Mwakilishi wa chama cha MPLA Manuel Agusto Alieleza, ushirikiano wa vyama hivi unaimarisha mataifa yao kwa kuenzi yale mazuri yaliyoachwa na waasisi.
Kwa upande wake mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) kutoka Mkoa wa Pwani, Hajji Jumaa alivishukuru vyama vya ukombozi kwa kushirikiana kuwezesha ujenzi wa chuo hicho na kuomba ushirikiano huo uendelee katika kuwezesha sekta nyingine za kiuchumi.
Uzinduzi wa barabara hiyo, ni mwelekeo wa uzinduzi wa chuo hicho, ambao utafanyika leo ambapo Mwenyekiti wa CCM na Rais Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
MARIAM MZIWANDA NA MWAMVUA MWINYI, Kibaha