WADAU wa baruti pamoja na wachimbaji wa madini nchini wametakiwa kufuata sheria ya baruti katika shughuli za biashara ya baruti na uchimbaji wa madini ili kuepusha madhara yanayoweza kujitokeza kama vile ajali na kupunguza nguvu kazi ya Taifa.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira wa Tume ya Madini, Mhandisi Henry Mditi, kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mhandisi Yahya Samamba, kwenye mkutano wa wadau wa baruti uliofanyika jijini Dodoma kwa lengo kujadili changamoto zinazojitokeza katika masuala yanayohusu baruti na kutafuta namna bora ya kuzitatua ikiwa ni pamoja na kuweka mikakati ya pamoja ya kusimamia sheria ya baruti na kanuni zake.
Amesema kuwa serikali imeweka mikakati mbalimbali ya kuhakikisha sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi, huku masuala ya usalama kwenye shughuli za uchimbaji wa madini yakipewa kipaumbele zaidi.
Ameongeza kuwa kuongezeka kwa shughuli za uchimbaji wa madini kumepelekea kuwepo kwa ongezeko la matumizi ya baruti hivyo Serikali kupitia Tume ya Madini imeweka mikakati ya kuzuia ajali za milipuko kwenye migodi ikiwa ni pamoja na kuhakikisha sheria, kanuni na taratibu zinazohusu masuala ya baruti zinafuatwa.
Amesema matumizi ya baruti hapa nchini yameongezeka kutoka wastani wa tani 3,000 kwa mwaka katika miaka ya 1990 hadi kufikia wastani wa tani 32,398 za baruti kwa mwaka 2021 kutokana na ongezeko la shughuli za uchimbaji wa madini, utafiti wa mafuta na gesi asilia na ujenzi wa miundombinu mbalimbali.
“Hadi kufikia sasa serikali imesajili jumla ya maghala 253 ya kuhifadhia baruti, na stoo na masanduku 470 ya kutunzia baruti katika migodi mbalimbali na sehemu za biashara, aidha kwa sasa zipo jumla ya kampuni 20 na watu binafsi 10 wanaojihusisha na uuzaji na usambazaji wa baruti hapa nchini” amesisitiza Mhandisi Mditi.
Katika hatua nyingine Mhandisi Mditi amesema kuwa Tume ya Madini itaendelea kutoa elimu kwa wachimbaji wadogo wa madini nchini kuhusu matumizi sahihi ya baruti ili kuhakikisha wanaendesha shughuli zao kwa kufuata kanuni za usalama.
Aidha, amewataka wadau wa baruti kuanzisha umoja wao ambao utatumika kama jukwaa la pamoja la kubadilishana uzoefu kwenye shughuli zao pamoja na kuwasilisha changamoto mbalimbali serikalini wanazokabiliana nazo kwenye utendaji kazi wa kila siku.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wadau wa baruti waliohudhuria mkutano huo wameipongeza Tume ya Madini kwa kuwa mkutano huo umetumika kama jukwaa la kuwasilisha changamoto zao kwenye shughuli za baruti.
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa baruti, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Orica Tanzania, Jimmy Ijumba ameomba sambamba na elimu kutolewa kwa wadau wa madini, huduma za baruti zisogezwe kwa karibu zaidi kwenye maeneo ya uchimbaji wa madini ili kupunguza mianya ya biashara haramu ya baruti.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Tansino Chemicals, Xinxin Qin amaipongeza Tume ya Madini kwa kuandaa mkutano huo ambao umetumika kama fursa ya kubadilishana uzoefu kwenye biashara na matumizi ya baruti.
“Hapa tumekutana wadau wa baruti kutoka sehemu mbalimbali nchini ambapo tumebadilishana uzoefu kwenye suala zima la utunzaji, matumizi na biashara ya baruti lengo likiwa ni kuhakikisha hazileti madhara kwenye matumizi yake na binafsi nimejifunza jambo kubwa sana,” amesema Qin.
Na MWANDISHI WETU