VIKUNDI na watu binafsi wanaojishughulisha ufugaji nyuki Halmashauri ya Mji wa Mbinga, mkoani Ruvuma, wametakiwa kuzingatia kanuni na utaratibu, ili wapate mazao bora na bei nzuri sokoni.
Akizungumza na UHURU mwishoni mwa wiki, Ofisa Nyuki wa Halmashauri hiyo, Gilbert Gotifrid, alisema wanaojishughulisha na ufugaji wa nyuki vipo vikundi 26 na watu sita binafsi, hivyo kujiingizia kipato.
Alibainisha kuwa ufugaji wa nyuki wa kisasa ni ule unaozingatia matumizi ya vifaa bora ambavyo huzalisha asali bora huku akisisitiza mafunzo humsaidia mfugaji kujua nyuki wanaofaa kufugwa.
Gotifrid aliongeza kwamba mwitikio umekuwa mkubwa kwa wafugaji nyuki kutokana na maelekezo yanayoendelea kutolewa mara kwa mara.
Hata hivyo, alisema kukosekana kwa elimu ya kutosha kwa muda mrefu, wananchi wa Wilaya hiyo walikuwa hawafugi nyuki huku kukiwa na mahitaji makubwa ya asali.
Aliwahimiza wanaofuga nyuki kuzingatia utunzaji wa mazingira kwa kuwa huwasaidia nyuki kupata chakula na maji na wahakikishe hawakati miti hovyo.
Akizungumzia umuhimu na faida za nyuki, Ofisa huyo alisema mbali na kusaidia kutunza mazingira, pia ni muhimu kwa maisha ya binadamu na viumbe hai vyote, kwa kuwa hufanya uchavushaji wa mimea.
Alizitaja faida za nyuki ni upatikanaji wa asali na nta, mazao ambazo zina faida kubwa hata katika soko la kimataifa, hutumika kama dawa ya kutibu baadhi ya magonjwa, utunzaji wa vyakula kama uokaji wa mikate, pia viwanda kutengenezea peremende.
Alisema asali inayozalishwa katika Halmashauri ya Mji wa Mbinga haijalisha soko la ndani, hivyo mkakati ulioko ni kuhakikisha wanaendelea kuongeza uzalishaji wa mazao yanayotokana na nyuki kwa kuelimisha jamii hususan wanawake na vijana ili wajikite na ufugaji wa nyuki.Å
NA DUSTAN NDUNGURU, MBINGA