NAIBU Waziri na Ujenzi na Uchukuzi, Mwita Waitara, ameutaka Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), kufungua dirisha la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu kazi zao.
Aidha, ameutaka wakala huo kuandaa vipindi mbalimbali kwenye runinga kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi na kujiongeza mapato.
Ameyasema hayo, alipozungumza na UhuruOnline, kuhusu mikakati ya TBA kufikisha huduma zao kwa jamii na kuongeza kuwa, wakala huo unatakiwa kufanya kazi kwa weledi na ubunifu, serikali ipate mapato yatakayosaidia utekelezaji wa miradi nchini.
Amewataka TBA kuwa wazi katika utendaji wa kazi, kuepusha maneno yanayoweza kuichafua taasisi hiyo, ambayo inafanya kazi kwa ubora kwa kuzingatia vigezo na masharti yaliyowekwa na serikali.
“Mnatakiwa kuwa wabunifu, muwe na miradi ya kuongeza mapato, lakini hili halitafanyika kama hamtajitangaza kwa ubora wenu na kutoa elimu kupitia vyombo vya habari,” amesema
Ameeleza kuwa, kwa sasa wizara zote zinatakiwa kuingia mikataba na TBA, katika ujenzi mpya wa mji wa kiserikali Dodoma, kwa hatua ya pili, hivyo wafanye kazi kwa ubora.
“Kuna uhaba wa nyumba za watumishi wa serikali Dodoma na baadhi ya nyumba zinahitaji ukarabati, hili liko chini yenu,” amesema.
Waitara amewataka baadhi ya watumishi wa serikali kuacha tabia ya kutokulipa kodi kwa sababu ni watumishi, lazima kuwe na makubaliano ya ulipaji kodi.
“Watumishi wenye tabia hii wanarudisha nyuma maendeleo ya serikali kwa kutokulipa kodi, wakijua ni haki yao kulipa kodi, lakini wanakuwa na visingizio mbalimbali,
Ameitaka TBA kuunda kamati ya kukusanya kodi kwa watumishi wa serikali, kwa kuangalia vigezo na masharti ya kila mtumishi kulingana na nyumba anayoishi.
Na ASHURA ASSAD