WAJASIRIAMALI wanawake wametakiwa kujitokeza kuchangamkia fedha za kupambana na Uviko-19, ambazo zimelenga makundi mbalimbali ikiwemo waanikaji madagaa, wakulima wa mwani, majongoo na Kaa.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais (anayeshughulikia kazi na uwezeshaji), Khadija Khamis Rajab amesema sh. bilioni 36 zilizotolewa na serikali zitakuwa chachu kwa wajasiriamali wakiwemo wanawake hususan katika mazao ya baharini.
Khadija alisema fedha hizo zinaratibiwa na Wizara ya Uvuvi zipo na wahusika wakiwemo wanawake wanatakiwa kuzichangamkia ikiwemo kujisajili katika makundi.
Pia alisema wakulima wa mwani 5,000 watanufaika na fedha hizo ambao wengi wao ni wanawake wa vijijini ambapo kunalimwa zao hilo kwa wingi.
Aidha waziri huyo alisema fedha hizo zimewalenga wakulima wa mazao ya baharini ya majongoo ya pwani 100 ambayo soko lake la uhakika.
Khadija alitoa wito kwa wananchi wa maeneo ya mwambao mwa baharini kuchangamkia ufugaji wa majongoo ya pwani ili kujiletea kipato na kuinua uchumi wa Zanzibar.
Aliwataka wananchi kujitokeza kuunda vikundi vya wajasiriamali watakaojisajili kuchangamkia fedha hizo ambazo zimelenga kuboresha miradi mingi ya kimkakati ikiwemo huduma za afya, barabara na elimu.
”Wafugaji mazao ya baharini changamkiani fedha za Covid-19 katika kujikomboa na ujasiriamali ili kupiga hatua kubwa ya maendeleo,”alisema.
Awali, Katibu Mkuu Wizara ya Uvuvi na Uchumi wa Buluu Dk. Aboud Suleiman Jumbe, alisema sehemu ya fedha zimetengwa kwa waanikaji wa madagaa 6,000 na kuwapatia vifaa vya kisasa vya kukausha samaki.
Aliwataka waanika madagaa kuhakikisha wanajisajili katika vikundi kwa ajili ya kutekeleza shughuli zao kwa mafanikio wakati wa kupata mgao wa fedha hizo.
Aidha aliwataka wakulima wa samaki aina ya pweza na kamba kutenga maeneo ambayo watahifadhi na kufuga kwa muda kwa lengo la kutoa mavuno mazuri.
”Tunawataka wavuvi wa pweza, ngisi na kamba kurudi katika utamaduni wa zamani wa kutenga maeneo ya uvuvi wa samaki kwa muda ili kutoa nafasi kuhakikisha wanapata mavuno mazuri,” alisema.
NA MWANDISHI WETU, ZANZIBAR