Na Sophia Nyalusi, Mtwara
MWENYEKITI wa Chama Kikuu cha Ushirika TANECU, Karimu Chipola, amewaomba wakulima wa Wilaya ya Newala na Tandahimba, kuendelea kulinda ubora wa ufuta ili kukuza pato la taifa.
Akizungumza katika mnada wa ufuta ambao umefanyika Wilaya ya Masasi, Chipola alisema mpaka sasa ufuta wa wilaya hizo mbili upo vizuri, lakini ni jukumu la kila mkulima kuendelea kulinda ufuta wake na siyo kuchanganya na mchanga.
Chipola alisema juhudi ya serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha wanunuzi wanafika kwa wakati na ndiyo maana kila mnada wanunuzi wanafika.
Alisema wakulima wana jukumu la kuleta ufuta msafi na mzuri ili wanunuzi waendelee kuwepo na kuongeza bei za ufuta na pato lizidi kuongezeka.
“Sitakuwa na mzaha kwa AMCOS yoyote ambayo haitafanya uhakiki wa ufuta ufikapo ghalani ili kuendelea kulinda ubora wa ufuta wetu na kuongeza pato la nchi kwa kuhakikisha unakuwa safi na hauna uchafu wowote,” alisema.
Meneja Mkuu wa TANECU, Mohamed Mwinguku, alisema kwa sasa wakulima wote wa Newala na Tandahimba wamelipwa zaidi ya sh. milioni 703 katika minada miwili, hivyo hakuna anayedai.
Alisema katika wilaya hizo wakulima wengi wanalima korosho na ndiyo maana walimaji wa ufuta ni wachache, hata hivyo waliolima zao hilo malipo yao yamefanyika kwa wakati.
Kwa mujibu wa Mwinguku, zao la ufuta kwa wilaya hizo mbili wamezalisha kilogramu 306,353 ambazo kwa minada hiyo wa kwanza bei ya juu ni sh. 2,250 na wa pili sh. 2,320 ambayo wakulima wamelipwa fedha zao.
Miongoni mwa wakulima wa ufuta, Wilaya ya Tandahimba, Joyce Chikota, alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wanunuzi wanakwenda kununua ufuta na kuwa wasichoke.
Naye John Alberto kutoka Wilaya ya Newala mkoani Mtwara, alisema juudi za serikali zinaonekana na kuomba wapelekewe pembejeo hatua ambayo itaimarisha zao la ufuta.