WAKULIMA wa korosho, Mkoa wa Pwani, wanatarajia kupata sh. bilioni 19.43 kutokana na mauzo ya msimu unaoendelea.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alibainisha hayo, mjini Kibaha, alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu mazao ya kibiashara.
Kunenge alieleza kuwa katika msimu huu, mkoa huo unatarajia kuvuna zaidi ya mara mbili tofauti na mwaka jana ambapo uliweka nguvu ili wilaya zinazolima zao hilo ziongeze uzalishaji.
Kwa mujibu wa Kunenge, hadi sasa fedha watakazopata wakulima ni za minada sita iliyofanyika Novemba 24, mwaka huu na mingine inaendelea.
Mkuu wa mkoa huyo aliweka bayana kuwa bei katika msimu huu, imeongezeka kutoka sh. 1,300 hadi kufikia sh. 2,040.
Aliongeza kuwa uzalishaji umeongezeka kutoka tani 7,000 na wanatarajia kupata tani 15,000, ambapo kati ya tani zilizouzwa 77.2 ni za daraja la kwanza na la pili ni 2,712.
Kunenge alibainisha kuwa kwa miaka iliyopita ilikuwa ni ngumu kupata korosho daraja la kwanza, lakini mwaka huu imepatikana huku bei yake ni kama iliyokuwa inauzwa Mtwara na Pwani.
Akizungumzia zao la ufuta, Kunenge alisema linainuka ambapo wamefikia tani 11,940 kutoka tani 7,000, hivyo kuwa msimu mzuri kwa wakulima wa zao hilo mkoani humu.
“Hayo ni mazao makubwa ya biashara katika mkoa wetu ambao unaendelea kuwahamasisha wakulima walime kwa kufuata kanuni bora za kilimo, kutumia wataalamu na pembejeo,”aliwahimiza.
Pia, aliwataka wakulima kutumia mvua zilizoanza kunyesha kwa kulima mazao yanayostawi kwa muda mfupi.
Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha