WAKULIMA wa zao la pamba nchini, wameshauriwa kutumia vipimo vipya vya kisasa, wakati wa upandaji ili kuwa na kilimo bora na chenye tija.
Wito huo umetolewa na Mratibu wa zao la pamba, Kituo cha Utafiti Ukiliguru, kilichopo Wilaya ya Misungwi, mkoani Mwanza, Dk. Paul Saidia, alipozungumza na Uhuru.
Alifafanua kuwa vipimo hivyo vitaleta mabadiliko na kuwaongezea idadi ya miche kutoka 22, 222 ya awali walipokuwa wakitumia vipimo vya sentimeta 90 kwa 40 kwa hekari moja na kufikia miche 444, 400 kwa kutumia vipimo vya sasa ambavyo ni sentimeta 60 kwa 30.
“Kwa ongezeko hilo la idadi ya mimea kwa hekari moja, mkulima atarajie kuongeza uzalishaji mara mbili ya ule wa awali, ambapo hekari moja ya pamba itamwezesha kupata kilo 2,000 kutoka kilo 1,000 na kumpaisha kiuchumi,” alisisitiza.
Mtaalamu huyo alieleza kuwa kuanzia mwaka 2017 walianza utafiti wa kilimo cha zao hilo katika mikoa mbalimbali nchini kwa kushirikiana na watafiti wa Chuo cha Lavras cha Brazil na kugundua upandaji wa zao hilo unaweza kubadilika na kuleta tija kwa wakulima na kuongeza kipato cha nchi.
Aliitaja baadhi ya mikoa waliofanyia utafiti huo kuwa ni Mwanza, Geita, Simiyu, Shinyanga na Mara, ambapo ilithibitika kupitia utafiti shirikishi wa vipimo vya sentimeta 60 kwa 30 utaongeza idadi ya mimea na kukua mara mbili ya vipimo vya awali.
Dk. Saidia alisema mkulima atakayepanda pamba kwa kuzingatia vipimo hivyo vipya na kufuata kanuni zinazosimamia kilimo bora cha pamba, atajiongezea kipato mara mbili na wala huo siyo muujiza ni utafiti wa vitendo uliobanisha.
“Mfano, mkulima mmoja wa kishapu (hakumtaja) alikuwa anavuna kilo 200 kwa eneo la ekari moja, baada ya kupata elimu ya upandaji kwa kutumia vipimo vipya, mwaka huu tulipomtembelea tulikuta amevuna kilo 224 kwa eneo la robo hekari,” alisema.
Hata hivyo, katika utafiti huo shirikishi changamoto walizokumbana nazo baada ya kuanza kampeni ya utafiti, ni pamoja na wananchi wengi kutokubali vipimo vipya kwa kuwa wamezoea upandaji wa kurusha wakati wakilima.
“Wakulima waliojitolea kwa moyo mmoja kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo, baadhi walivunjwa moyo kwa maneno ya wenzao waliokuwa wakiwambia kuwa wanapoteza muda wao bure, waliovumilia wameona manufaa yake,” alibainisha.
Dk. Saidia alitoa wito kwa wakulima kuwa mbali na kutumia vipimo hivyo, wanapaswa kutumia viua wadudu na mbolea asilia katika upandaji wa pamba kwa kuwa zao hilo linahitaji virutubisho kutoka katika udongo.
NA BLANDINA ARISTIDES, Misungwi