WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mohamed Mchengerwa, ametoa wiki mbili kwa Wakurugenzi wa Halmashauri, kuwasilisha ofisini kwake orodha ya maofisa utumishi walioshindwa kuwapandisha madaraja watumishi wa umma 96,000.
Mchengerwa alitoa agizo hilo jana jijini hapa wakati akifungua mkutano wa tisa wa Chama cha Taaluma ya Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA).
“Baada ya kupandisha watumishi madaraja kumalizika, tulipata malalamiko, tumetoa nafasi nyingine 96,000 za walioachwa kupandishwa, lakini linasuasua.
“Sasa Wakurugenzi wasilisheni ofisini kwangu majina ya orodha za maofisa utumishi walioacha baadhi ya majina ya watumishi wenzao waliokuwa na sifa za kupandishwa madaraja, lakini waliwaacha kutokana na nongwa zao,” alieleza.
Kwa mujibu wa Mchengerwa, baadhi ya maofisa utumishi wanaojifanya miungu watu na wengine kukwamisha watumishi wenzao wasipande madaraja au kudai stahiki zao kwa sababu ya vyeo walivyonavyo, huku wakisahau vyeo ni dhamana, hawatavumiliwa.
Naye Katibu wa TRAMPA, Fransice Mathias, alisema mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 ulisababisha mkutano huo kutofanyika mwaka jana, hivyo kulazimika kuufanya mwaka huu kwa tahadhari.
Alieleza kuwa, mkutano huo umehudhuriwa na watunza kumbukumbu na nyaraka zaidi ya 2,400 nchi nzima.
Pia, alisema mrundikano wa nyaraka katika taasisi za umma, ukosefu wa ofisi za masijala za siri, kupitwa na wakati muundo wa utumishi wa umma wa mwaka 2021 ni miongoni mwa changamoto zinazoikabili kada hiyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Makatibu Mahsusi (TAPSEA), Zuhura Maganga, alisisitiza nidhamu ya kazi na utunzaji siri kwa watunza nyaraka na kutoa rai kwa kada hiyo kutoingiza siasa katika chama hicho.
Alieleza kuwa ni muhimu wakitumie chama hicho kama jukwaa la kutatua changamoto zinazowakabili
kwa kushirikiana na serikali ili waweze kuzitatua.
ATOA AGIZO TAKUKURU
Katika hatua nyingine, Mchengerwa aliitaka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia utekelezaji wa miradi yote ya Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF), awamu ya nne itakayotekelezwa katika mikoa ya Arusha, Mwanza, Njombe, Geita na Simiyu.
Akifungua kikao kazi cha siku mbili jijini hapa cha utekelezaji wa awamu ya nne ya mradi ya TASAF, Mchengerwa alisema serikali imetoa kiasi cha sh. bilioni 130 kwa halmashauri zote za mikoa hiyo ambazo zitatumika kuboresha maisha ya wananchi kupitia miradi watakayoibua, hivyo hategemei kusikia ubadhirifu wa aina yeyote.
“TAKUKURU timizeni wajibu wenu, hakikisheni mnakuwa macho muda wote katika kufuatilia miradi yote ya TASAF itakayokuwa inatekelezwa katika maeneo yenu kwa sababu lengo la serikali ni kuwakomboa wananchi wanyonge, wajikwamue kiuchumi,” alieleza.
Alisema miradi hiyo, itakuwa kipimo cha kuwapima watendaji wote wa ngazi ya wilaya na mkoa kama wanatekeleza majukumu yao kikamilifu katika kuzisadia kaya masikini kupitia fedha za TASAF.
Mchengerwa alitumia fursa hiyo kuwataka wenyeviti wa halmashauri katika kila wilaya kusimamia miradi hiyo kwa weledi kwa sababu wao ni sehemu ya uwakilishi wa wananchi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga, alisema madhumuni ya kikao hicho ni kujengeana uelewa wa shughuli za TASAF ambapo utekelezaji umekua wa mafanikio na kusisisitiza kuwa wameboresha programu mbalimbali katika awamu ya nne ya mradi.
“Katika awamu hii, tumeboresha programu mbalimbali zikiwemo za kufahamu mabadiliko na majukumu sahihi ya utekelezaji ili kuongeza tija na kupatikana miradi mingine endelevu na taarifa sahihi kutolewa kwa wananchi katika usimamizi, utekelezaji na ufutailiaji wa miradi katika maeneo yao,” alibainisha.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, aliishukuru TASAF kwa kutoa sh. biloni 1.5 katika awamu iliyopita ambapo awamu ya nne fedha zilizokuja ni nyingi kuliko kasi ya utendaji kazi, hivyo Mkoa utasimamia na kudhibiti matumizi yake.
Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini (CCM), Mrisho Gambo, alisema TASAF ni mkombozi wa wananchi wanyonge ambao wananufaika kupitia mradi mbalimbali, hivyo alisisitiza maeneo ambayo hayajaibuliwa yataingizwa katika mpango huo.
Na LILIAN JOEL, Arusha