BAADHI ya wananchi Zanzibar, wamesema wapo tayari kuungana na serikali katika mapambano ya wimbi la tatu la ugonjwa wa covid 19, ikiwemo kujitokeza kupata chanjo.
Pia, wamewasihi wengine wenye dhana potofu kuhusu chanjo hiyo, kuachana nayo badala yake waiamini serikali kwa kuwa haiwezi kuwaletea chanjo ambayo siyo salama kwa afya zao.
Wananchi hao waliyasema hayo kwa nyakati tofauti wakati wakizungumza na UhuruOnline. Moja wa watu hao ni mkazi wa Mji Mkongwe, Zanzibar, Ahemd Al-wahab, ambaye alisema yupo tayari kwenda kuchanja chanjo hiyo na kuwataka wananchi kuacha dhana ya kwamba siyo salama.
“Nina uhakika kuwa serikali yangu imeichunguza ipasavyo chanjo hii na ndiyo maana ikaletwa nchi kwa ajili yetu ili wananchi tupate, kwa kuwa ni salama kwa maradhi haya,” alisema.
Aliwaomba wananchi kujiuliza jambo moja ambalo ni kwamba serikali itanufaika vipi endapo itawaletea wananchi wake chanjo ambayo siyo salama kwa afya zao.
“Haiwezekani wala haiingii akilini kwamba viongozi wetu wakubwa wawe na lengo la kutuumiza sisi wananchi wake, kwa sababu kutakuwa hakuna faida kwao ya kufanya hivyo. Niwasihi tu wananchi wenzangu kuchukua tahadhari zote za corona na kwenda kupata chanjo pale utaratibu utakapotangazwa,” alisema.
Kwa upande wake, Sabra Ali Suwed, mkazi wa Mbweni, Zanzibar, aliishukuru serikali kwa kuwajali wananchi na kuleta chanjo ya maradhi hayo, ambayo ni hatari duniani.
Aliomba utolewe utaratibu kwa wananchi wa kawaida ili wapate huduma hiyo ya chanjo, ambayo kwa sasa inatolewa kwa makundi maalumu ya watu.
Alitoa wito kwa wananchi ambao bado wana dhana potofu ya kusema chanjo hiyo siyo salama na kwamba mtu akichanjwa basi atapata madhara, kuondokana na dhana hiyo, badala yake waiunge mkono serikali.
Naye, Ali Rahid Machano, mkazi wa Kwa Mchina, alibainisha kwamba iwapo chanjo hiyo siyo salama, basi hata viongozi wa juu wa serikali wasingechanjwa, huku akimtolea mfano Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ambaye hivi karibuni alipata chanjo mbele ya Watanzania wote.
Pia, alisema wapo viongozi mbalimbali wa Tanzania bara na hata wa Zanzibar, tayari wameshapatiwa chanjo hiyo, jambo linaloashiria kuwa ni salama kwa wananchi.
Utoaji wa chanjo Kisiwani Unguja unaendelea katika eneo maalumu lililotengwa la Shule ya Sekondari Lumumba, ambapo awamu hii wanachanjwa watumishi wa sekta ya afya na makundi maalumu ya wananchi wenye matatizo ya afya.
EMMANUEL MOHAMMED Na HANIFA RAMADHANI, ZANZIBAR