BAADHI ya wanaume wilayani Iringa, Mkoa wa Iringa, wameiomba serikali kuwanusuru dhidi ya vitendo vya ukatili wanavyodai kutendewa na wake zao, ambao wamekuwa wakiwapiga na kuwaathiri kisaikolojia.
Ombi hilo wamelitoa walipozungumza katika mkutano wa Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Mohamed Moyo, alipokuwa akisikiliza kero za wananchi kwa lengo la kuzibaini na kuzipatia ufumbuzi.
Akizungumza mbele ya mkuu huyo wa wilaya, mkazi wa Kijiji cha Kiponzelo ambaye alikataa kutaja jina lake, alisema kuna haja ya kuwepo dawati maaalumu la utetezi wa haki za wanaume na usaidizi wa kisaikolojia ili kuwaepusha na msongo wa mawazo.
Alimweleza mkuu wa wilaya ya Iringa kwamba wake zao katika kijiji hicho wamekuwa na tabia ya kuwafanyia ukatili kwa kuwapiga na kuwasimanga hadharani mara kwa mara.
“Lakini jambo la kushangaza tunapotoa taarifa kwa viongozi wa serikali za vijiji na kata ili kupata usaidizi, hatuoni hatua za moja kwa moja kuchukuliwa,” alieleza.
Alidai kuwa kushamiri kwa vitendo hivyo kuna wafanya baadhi ya wanaume kutenda ukatili mkubwa kwa wake zao kama hatua ya kulipiza kisasi na kusababisha uhasama kuendelea ndani ya jamii.
“Kwa kweli wanaume tunapigwa sana, yaani tunafanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia na tunashindwa kutoa taarifa kutokana na mila zetu sisi Wahehe,” alidai mwanaume huyo.
Akijibia malalamiko hayo kwa niaba ya Kamanda wa Polisi, Wilaya ya Iringa, Mkuu wa Kituo cha Polisi Ifunda, Agustino Malema, alisema kuwa polisi wameanzisha kitengo cha dawati la jinsia ambalo linahusika na matukio kama hayo.
Alisema hakuna Mtanzania anayetakiwa kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsi kwa kuwa mara nyingi kitendo hicho kimekuwa kikiwaathiri kisaikolojia na kupunguza ufanisi wa akili.
“Niwaombe wananchi mnaofanyiwa vitendo hivyo, mnatakiwa kutoa taarifa polisi bila aibu ili kumaliza tatizo hili ambao limekuwa linaibuka kwa kasi,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Moyo, alisema moja ya ajenda yake ni kutoa elimu ya kupinga unyanyasaji wa kijinsia kwa wananchi wa wilaya hiyo.
Alisema Wilaya ya Iringa inaongoza kwa vitendo vya ukatili wa kijinsia, hivyo ni lazima watafute njia ya kukomesha vitendo hivyo ambavyo vinakuwa vikiharibu sifa nzuri ya wilaya hiyo.
Mkuu wa Wilaya aliwaagiza wenyeviti wa vijiji na watendaji kuhakikisha wanafichua vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kuwaondoa waathirika katika msongo wa mawazo ambao wanakumbana nao mara baada ya kufanyiwa vitendo vya ukatili wa kijinsia
“Kitendo cha kumpiga mtu ni kosa la jinai, ukigundulika sheria itafuata mkondo wake, niwatake wananchi kwenda kuripoti matukio haya ya ukatili wa kijinsia katika vyombo vinavyohusika,”
“Niwaombe wananchi mnaofanyiwa vitendo hivyo, mnatakiwa kutoa taarifa polisi bila aibu ili kumaliza tatizo hili ambao limekuwa linaibuka kwa kasi”. Mkuu wa Wilaya Mohamed Moyo.
Na CATHERINE MBIGILI, Iringa