RAIS Samia Suluhu Hassan ametangaza uamuzi wa kuunda wizara maalum itakayoshughulikia masuala ya maendeleo ya wanawake na watoto kwa dhumuni la kuwezesha usimamizi, uratibu na ufuatiliaji wa sera zinazohusu masuala ya wanawake nchini.
Amesema atamshauri pia Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Dk. Hussein Ali Mwinyi, kuunda wizara hiyo visiwani Zanzibar.
Rais Samia alitoa maagizo hayo Desemba 16, 2021 jijini Dodoma wakati akizindua Kamati ya Ushauri ya Kitaifa kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi chenye usawa, uzinduzi uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, dini, mabalozi, viongozi wa vyama vya siasa na wananchi.
“Ndugu zangu unaweza kuona kwamba pamoja na jitihada zote tulizozifanya, mipango na sera zote tulizoweka, bado hatujafika tulipotakiwa kufika. Sasa ili tuweze kufika tunapotakiwa kufika, lazima kuwe na usimamizi, uratibu, kutathmini na ufuatiliaji wa sera na utekelezaji wetu wa mipango.
Aliongeza kuwa: “Uamuzi wangu ni kuitenga wizara itakayoshughulikia jinsia, maendeleo, wanawake na mambo mengine, kutoka katika kuchanganywa na wizara ya afya kwa sababu tukiweka wizara ya afya na mambo mengine na hali tuliyonayo sasa duniani, sekta ya afya pekee yake inachukua sura kubwa ya wizara hii kuliko vipengele vingine vilivyobaki.”
Rais Samia alisema: “Kama tutatenga vipengelee vingine vilivyobaki na afya tukaisimamisha pekee yake, usimamisizi wa sera, sheria na mambo mengine unaweza ukaenda vizuri na ukapata msukumo unaohitajika. Kwa hiyo hayo ndio maamuzi yangu na nitajaribu kumshawishi Rais wa Zanzibar naye afanye hivyo hivyo ili twende vizuri.”
Kuhusu kamati hiyo, alisema kamati hiyo ina jukumu ya kuhakikisha taifa linafikia haki za usawa wa kiuchumi, hususan kwa wanawake na kuondokana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.Rais Samia alitoa maagizo kwa mawaziri, wakuu wa mikoa, wakurugenzi pamoja na taasisi zote za wizara, kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika utekelezaji wa ahadi hizo.
Pia, alitoa maagizo kwa kamati hiyo kuhakikisha inatoa ushauri bora wa namna ya ushirikishwaji wa wadau wa kimkakati na kushiriki shughuli za utoaji elimu katika jukwaa la usawa kwa wananchi.
“Nimekubali kutekeleza eneo hilo kutokana na kazi waliyoifanya mwaka 2016 kuwa wajumbe wa jopo la kumshauri Ban Ki-Moon aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa,”alisema.
Alieleza kuwa jukwaa hilo ni mwendelezo wa jukwaa la Umoja wa Mataifa katika kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma katika kutekeleza lengo namba tano la milenia.
Rais Samia alisema ili kumuinua mwanamke kiuchumi, mambo mbalimbali yanahitajika kutekelezwa kwani wanawake ambao ndio nguvu kazi ya taifa bado ni waathitirika wa kiuchumi.
“Bado sehemu kubwa ya Dunia haijatoa nafasi stahiki katika kuwatumia wanawake ili kuchangia uchumi wa Dunia kwani wanawake wakitumika vyema inakadiriwa watachangia sh. trilioni 21 kwa mwaka,”alieleza.
Alisema muda umefika kufanyia kazi sera, sheria na mipango inayowekwa katika kuleta usawa wa kijinsia.
“Serikali inatekeleza mikataba ya maazimio ya kikanda ikiwemo wa mwaka 1978, Mkataba wa mtoto wa 1989 na Mkataba wa Haki na Ustawi wa mtoto wa Mwaka 1989,” alibainisha.
Kwa upande wake, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alimhakikishia Rais Samia kuwa watasimamia na kufuatilia uratibu wa jukwaa hilo ili kufikia malengo ya utekelezaji wake.
Majaliwa alitoa rai kwa wadau kuona namna ya kuzingatia ahadi za kitaifa na mikakati ya utekelezaji wa malengo ya pamoja.
Awali, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima, alisema kuwepo kwa kamati hiyo itasaidia kasi ya utekelezaji mpango wa taifa wa ahadi za nchi, kwani jukwaa hilo ni utekelezaji wa maazimio ya Beijing ya mwaka 1995 na ilionekana ni muhimu kuweka kasi ya utekelezaji wa masuala ya kijinsia.
Kamati hiyo ya kitaifa kuhusu utekelezaji wa ahadi za nchi katika jukwaa la kizazi cha usawa wa kijinsia, ina wataalamu 25 ambapo Mwenyekiti wake ni Angela Kairuki.
Na Happiness Mtweve, DODOMA