WANAWAKE wawili wamekamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Abeid Amani Karume kwa nyakati tofauti wakituhumiwa kusafirisha dawa za kulevya kwenda nchi za nje.
Akizungumza na waandishi wa habari, Naibu Kamishna wa Upelelezi na Makosa ya Jinai (DCI) Zubeir Chembela, amesema mtuhumiwa Sabah Mbaraka Mbarouk (39) mkazi wa Makorora Tanga, alikamatwa uwanjani hapo wiki iliyopita akiwa na kilo 1.6 za dawa hizo zinazokisiwa ni aina ya Heroine zikiwa katika begi lake.
Chembela amesema Sabah alikamatwa usiku saa 5:15 akiwa katika hatua za mwisho kwenda kupanda ndege ya Shirika la ndege la Qatar Airways kuelekea nchini India.
“Huyu ni mwenyeji wa Makorora Mkoa wa Tanga tulimkamata katika uwanja wa ndege wa kimataifa na kikosi cha kupambana na dawa za kulevya akiwa katika hatua za mwisho kusafiri kuelekea India,” alisema.
Aidha, Chembela amesema kuwa Januari 31, mwaka huu, Rehema Mwinyimkuu Mohamed (31) mkazi wa Kinondoni mwenye umiliki wa hati ya kusafiria namba TAE 447433, alikamatwa na dawa za kulevya pia zinazokisiwa aina ya Heroine zenye uzito wa kilo 4.36 zikiwa katika begi lake.
Rehema alikuwa akitoka Afrika Kusini kwa kutumia ndege ya Ethiopia Airline na alikamatwa katika jengo la abiria la Terminal III baada ya kutiliwa shaka na wafanyakazi wa uwanja huo.
“Abiria Rehema Mwinyimkuu tulimkamata akitokea Afrika Kusini kwa kutumia ndege ya Shirika la ndege la Ethiopia Airline akiwa na kilo 4.36 na kwa sasa watuhumiwa wote tunawashikilia tukisubiri kukamilika kwa baadhi ya taratibu kufikishwa mahakamani,” alisema Chembela.
NA KHATIB SULEIMAN, ZANZIBAR