WAKAZI wanne wa jijini Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kujibu tuhuma za wizi wa vitu mbalimbali kwa unyang’anyi wa kutumia silaha.
Washitakiwa hao ni Rajabu Rajabu (23), Rajabu Zengo (28), Proches Paschal (42) na Said Mohammed (28) ambao walisomewa shitaka hilo juzi na Wakili wa Serikali, Hilda Katto, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Easter Mwakalinga.
Hilda amedai washitakiwa hao, walitenda kosa hilo Februari 3, mwaka huu, eneo la Mbezi Malamba Mawili iliyopo wilayani Ubungo, Dar es Salaam.
Amedai washitakiwa hao, waliiba vitu mbalimbali vikiwemo milango 16 yenye thamani ya sh.320, 000, soketi ‘breaker,’ fedha taslimu sh. milioni 1.88 vyote vikiwa mali ya Shabani Issa.
Inadaiwa washitakiwa hao, kabla na baada ya kutenda kosa hilo, walimtishia Twaha Abdallah kwa panga ili wajipatie mali hizo.
Washitakiwa hao walikana kutenda kosa hilo, upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji kwa awali.
Hakimu aliwaeleza washitakiwa kwamba, shitaka halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo watarudi mahabusu na shauri liliahirishwa hadi Septemba 20, mwaka huu.
EVODIA MICHAEL (UDSM), DAVID KOMBA
(TUDARCo) na HAWA NGADALA