SIKU moja baada ya kutokea ajali ya mlipuko wa moto katika kituo cha kupokea na kupooza umeme, Msamvu, mkoani Morogoro, Waziri wa Nishati, Dk. Medardi Kalemani, amewasimamisha kazi watumishi wanne kupisha uchunguzi.
Waziri Kalemani, ametoa agizo hilo, baada ya kutembelea eneo la mlipuko, ambapo ameagiza kusimamishwa kazi watumishi hao ili vyombo husika vifanye uchunguzi na hatua nyingine zichukuliwe.
“Hatuwezi kukubali kuona mambo kama haya yanafumbiwa macho, hivyo nimeagiza kusimamishwa kazi watumishi hawa, kupisha uchunguzi kwani lengo ni kuona kitendo hiki hakijirudii,” amesema Dk. Kalemani
Amesema chanzo cha moto huo ni ujenzi wa reli ya mwendo kasi unaoendelea eneo la Tungi, Manispaa ya Morogoro, ambapo tingatinga lilichimbua nyaya za umeme na kusababisha mlipuko katika kituo hicho na hasara ya zaidi ya sh. bilioni mbili.
Watumishi waliosimamishwa, watatu wa Shirika la Umemem (TANESCO), ambao ni wasimamizi wa kituo hicho na mmoja ni msimamizi wa ujenzi wa reli hiyo, Kituo cha Tungi na kwamba, uchunguzi utafanyika kwa siku tano.
“Nimeagiza uchunguzi huu kufanyika ndani ya siku tano na kama watu hawa watakutwa na hatia, watachukuliwa hatua za kisheria, lakini kama wataonekana hawana, watarudishwa kazini kuendelea na majukumu yao,” amesema.
Aidha, ameagiza TANESCO Mkoa wa Morogoro, kuweka alama maeneo yote yenye miundombinu ya umeme, itambuliwe kirahisi na kuepusha kujirudia kwa matukio hayo.
Mbali na hilo, Dk. Kalemani ameitaka TANESCO mkoani humo, kuhakikisha maeneo yote, ambayo hayana huduma ya umeme kutokana na mlipuko wa juzi, yanarejeshewa umeme ndani ya saa 24, kazi za uzalishaji mali ziendelee.
Kwa upande wake, Meneja wa TANESCO, Mkoa wa Morogoro, Mhandisi Fragrance Shuma, amesema ajali hiyo imesababisha hasara kubwa kwa shirika kwani kituo hicho kimeungua kwa asilimia kubwa.
Amesema mbali na kituo hicho cha kupokea na kupoza umeme kuungua kwa asilimia kubwa, mitambo yake ni mizima na kwamba, watahakikisha huduma ya umeme kwa wananchi inarejea ili kutokwamisha uzalishaji mali.
Na WARIOBA IGOMBE, MOROGORO
