ROBO tatu ya wananchi wa kijiji cha Lukale kilichopo kata ya Bukundi wilayani Meatu mkoani Simiyu, hawajui kusoma wala kuandika hatua iliyopelekea kumuomba Mkuu wa Mkoa David Kafulila, vituo vitatu vya elimu ya watu wazima sambamba na walimu.
Ombi hilo limetolewa na Mwenyekiti wa kitongoji cha Dumanang, kilichopo kijijini hapo Girahuda Gisura, mbele ya mkuu wa mkoa, huku akiongeza kuwa kijiji hicho kipo umbali wa zaidi ya kilometa 80 kutoka makao makuu ya wilaya ya Meatu na wananchi wake wakijishughulisha na kazi za uchimbaji madini ya chumvi yaliyopo ndani ya kijiji hicho sambamba na ufugaji na kilimo.
“Robo tatu ya wananchi wa kijiji cha Lukale hawajui kusoma wala kuandika, … serikali itupatie angalau vituo vitatu vya MEMKWA, ili wananchi wanufaike angalau wajue kusoma na kuandika,” amesema Gisura
Naye mtendaji wa kijiji hicho, Michael Kilatu, amesema kijiji hicho kina takribani wananchi 1699 huku akikiri kuwepo kwa idadi kubwa ya wananchi ambao hawajui kusoma na kuandika huku akiongeza kuwa katika kuchangia shughuli za maendeleo wapo mstari wa mbele na wana mwitikio mkubwa.
Kwa upande wake RC Kafulila, baada ya kupokea ombi hilo amemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo pamoja na Afisa Elimu Msingi kuhakikisha wanaleta walimu na kuanzisha kituo cha elimu ya watu wazima ndani ya kijiji hicho kwa hitaji la wananchi hao.
Na Anita Balingilaki ,Simiyu