MKUU wa Chuo Kikuu Cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Jaji Mstaafu Joseph Warioba, amewataka wataalamu wa kilimo nchini kutoa elimu ya kilimo biashara, kuwezesha taifa kukabiliana na mahitaji ya chakula kutokana na ongezeko la watu duniani.
Jaji Warioba aliyasema hayo, mjini Morogoro alipotembelea miradi ya chuo hicho ukiwemo wa Hospitali ya Rufaa ya Wanyama.
“Kabla ya Uhuru Watanzania tulikuwa milioni tisa, lakini sasa tupo milioni takribani 60, hivyo miaka arobaini ijayo huenda tukafikia milioni 100. Ipo haja kwa wanafunzi wanaojifunza kilimo biashara kuhakikisha utaalamu huo wanausambaza nchini ili uwasaidie wengine katika kuzalisha kilimo biashara kulingana na ongezeko la watu,” alisisitiza.
Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Raphael Chibunda, alisema SUA kwa kushirikiana na taasisi ya Private Agricultural Sector Support (PASS), wameanzisha kozi maalumu ya kuwaendeleza wanafunzi wa kada mbambali kuhusu kilimo biashara.
Alisema wametenga sh. milioni 450 ya kujenga vitalu nyumba 30 vitakavyowapangisha wahitimu hao kwa ghArama nafuu ili wajiendeleze baada ya kuhitimu mafunzo ya mwaka mmoja katika kozi hiyo.
“Matarajio yetu tuwe na vitalu nyumba 100 na PASS wanavyo 100, hivyo kuwa na idadi ya vitalu nyumba 200,” alisema.
Chibunda alitoa wito kwa wafugaji pale wanapoona mifugo yao ina magonjwa ambayo yameshindikana, wafike SUA katika hospitali ya rufaa ambayo ndio pekee nchini kupata matibabu.
“Kwa sasa tuna mashine ya “Utrasound” ambayo tunaweza kutambua magonjwa ya wanyama kwa urahisi na kutoa tiba, tuna wataalamu waliobobea katika fani hiyo,” alisema.
Naye, Mkuu wa Idara ya Upasuaji na Uzalishaji Wanyama, Profesa Modesta Makungu, alisema wanyama kama mbwa wana magonjwa yanayofanana na binadamu, hivyo kuwepo kwa mashine ya ‘utrasound’ itasaidia kurahisisha kujua magonjwa kwa urahisi.
NA LATIFA GANZEL, MOROGORO