WAZIRI Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ameng’aka na kusema jamii ya Watanzania, inapaswa kuwakemea kwa nguvu zote wanaotaka kuleta ubaguzi miongoni mwao kwa sababu hawana nia njema na Tanzania.
Jaji Warioba amesema udini, ukabila, ukanda, uvyama katika kipindi cha hivi karibuni, vimeonekana kuzungumzwa kwa kiwango kikubwa, hali inayoweza kuhatarisha misingi ya amani ya taifa iliyoasisiwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.
Aliyasema hayo Dar es Salaam, kama sehemu ya hotuba yake wakati akifungua Kongamano la Kumbukizi ya miaka 22 ya kifo cha Hayati Mwalimu Julius Nyerere, lililofanyika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.
“Viongozi tukemee wanaotaka kuleta hayo (Ya kibaguzi), Watanzania tuwe kitu kimoja, tufanye mambo yetu, kuijenga nchi yetu,” alisema.
Kauli yake, imekuja siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan, akemee ubaguzi unaoonekana kuzungumzwa na baadhi ya watu, wakiwemo viongozi hasa linapokuja suala la uwajibishwaji katika utumishi wa umma.
Waziri mkuu huyo mstaafu alisema amani imejengwa kwa jasho na kwamba, haikupatikana kwa mara moja, hivyo jamii isiruhusu kuchezewa kwa tunu hiyo ambayo imeendelea kuwepo nchini kwa kipindi kirefu.
“Juzi Rais (Samia), aliongea mambo haya, kukemea udini, ukabila, ukanda na uvyama, nilimhurumia hii ni misingi ya umoja wetu, ambayo imeanza kuchezewa.
“Amani haikuja hivihivi, ilijengwa pamoja na umoja na hizi ni moja ya kazi za mwanzo kabisa alizozifanya Mwalimu wakati wa uongozi wake kwa taifa hili.
“Mwalimu alitaka kuondoa ukabila na aliishi hivyo, marafiki zake wa karibu, ukimzungumzia Mzee Kawawa, alikuwa ni muislamu, yeye alikuwa mkristo, mkatoliki,” alisema.
Kadhalika, alisema uadilifu wa Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake haukuwa na shaka, kwamba hata maadui zake walidiriki kukiri juu ya sifa hiyo ya Mwalimu.
Alisema Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake aliishi maisha ya kawaida, yasiyo na mbwembwe na alithamini utu na haki kwa wote.
Jaji Warioba ambaye aliwahi kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa utawala wa Nyerere, alisema wakati taifa linakumbuka miaka 22 ya kifo chake, linapaswa kuishi matendo yake badala ya yanayoandikwa kumhusu.
“Ninatamani sote tufahamu kuwa maisha yake aliyoyaishi ni muhimu tukajifunza kuyahusu kuliko kumbukumbu za kifo chake,” alisema.
Alisema Mwalimu pamoja na kuwa mtoto wa chifu na nafasi kubwa aliyopewa katika jamii, bado alibaki mtu wa kawaida mwenye mawazo na mwelekeo wa mtu wa kawaida.
Jaji Warioba alisema Mwalimu alikuwa na imani ya utu wa binadamu, aliamini watu wote ni sawa kwamba kila mtu anastahili heshima.
“Mwalimu alipochaguliwa kuwa Rais, wakati ule ilikuwa ni kawaida watu kumuita mtukufu Rais, lakini yeye alikataa kuitwa mtukufu Rais, akasema yeye si mtukufu, mtukufu ni Mungu, yeye ni binadamu na mwalimu wa kawaida. Ndio chanzo cha kumuita Mwalimu,” alisema Jaji Warioba.
Pia, alisema mkewe Maria Nyerere, ilikuwa kawaida wakimuita ‘First Lady’, lakini alikataa na kusema huyu ni Mama Maria, ndio jina hilo limekua kama cheo.
Jaji Warioba alisema Mwalimu alikataa jina lake kutumiwa kwa mambo mbalimbali, kama majina ya barabara, majengo na kwamba, alipokuwa Rais hakukuwa na barabara iliyokuwa na jina lake.
Alisema Mwalimu hakupenda viongozi kuitwa mheshimiwa, aliamini Watanzania wote ni ndugu na alitaka waitane ndugu ikiwamo yeye kuitwa ndugu Rais.
“Wakati wake, kumuita ndugu Rais ilikuwa jambo la kawaida. Uhusiano wake ni kweli alikuwa anafanya kazi na viongozi, lakini hakusahau marafiki zake wa kawaida na alikuwa anakutana nao na wazee wanacheza bao pale Msasani na kunakuwa na utani mwingi.
Jaji Warioba alisema Mwalimu Nyerere alikuwa anaamini haki kwa wote, hata katika maandiko yake alikuwa anasisitiza haki na ndiyo ulikuwa msingi kwenye mapambano ya kujikomboa kutoka kwa wakoloni.
Alisema Tanzania ina zaidi ya makabila 120, lakini Mwalimu Nyerere alitumia lugha ya Kiswahili kuyaunganisha makabila yote kwa kujenga, umoja, mshikamo na hadi sasa nchi ina amani.
“Ili kuheshimu hili, ufike wakati elimu yetu yote iwe kwa lugha ya Kiswahili,” alisema Jaji Warioba.
Naye Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (Mwalimu Nyerere Foundation), Joseph Butiku, akizungumza katika kongamano hilo, alikemea mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa umma, ili kuendelea kulinda mafundisho ya Mwalimu Nyerere.
“Ukiwa na nafasi ya uongozi, unatakiwa utambue ile ni dhamana, uongozi ni dhamana, kwamba vitu ulivyopewa uvisimamie si vyako, ni vya wote.
“Weka utaratibu wa kuvitumia kwa faida ya watu wote sio kwa ajili ya mtu fulani au kikundi cha watu fulani na wengine unawasahau,” alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere, Stephen Wasira, akichangia mada za kongamano hilo, alisema chuo hicho kimekuwa na utamaduni wa kuandaa makongamano hayo mara tatu kwa kila mwaka kwa Tanzania Bara na Visiwani.
Akimzungumzia Mwalimu Nyerere, alisema katika uzoefu wake wa kisiasa, hamfahamu kiongozi mwingine wa kumlinganisha na Mwalimu Nyerere kimaadili.
“Alikuwa wa kawaida kabla ya uongozi, akiwa uongozini na hata baaa ya uongozi, hakuwaibia wananchi,” alisema Wasira.
Kongamano hilo lililoongozwa na Mada kuu: ‘Maono ya Mwalimu Nyerere katika uongozi, maadili, umoja na amani kwa maendeleo ya jamii’ lilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa, kisiasa, wananchi na wanataaluma.
Na WILLIAM SHECHAMBO