WAZIRI wa Afya, Ummy Mwalimu, amesema pamoja na serikali kuchukua hatua za haraka katika mapambano dhidi ya UVIKO- 19, ikiwemo kuhimiza kuchanja hali hairidhishi ambapo hadi kufikia Januari 25 mwaka huu, ni asilimia tatu pekee ya wananchi waliochanja.
Aidha vifo vitokanavyo na ugonjwa huo vimeongezeka, ambapo kati ya vifo 76 vitokanavyo na Corona 73 ni watu wasiochanja.
Amesema ni muhimu jamii kutambua kuwa, Corona ipo na ni hatari kwa watu wasiochanja na hadi kufikia Januari 23 mwaka huu watu 33,000 wamethibitika kuwa na ugonjwa wa UVIKO-19 nchini na watu 781 wamepoteza maisha kutokana na ugonjwa huo.
Hatua hiyo imesebabisha kuwa na takwimu za hadi Januari 25 mwaka huu, watu 1922,019 pekee ndio waliochanja kati ya Watanzania wote.
Aidha, kufikia Januari 23 mwaka 2022, jumla ya wagonjwa 3,147 walilazwa kutokana na ugonjwa wa Uviko-19 kati yao 2,990 walikuwa hawajachanja huku kati ya wagonjwa mahututi 31 walioripotiwa 30 hawakuchanja na kati ya vifo 76 vilivyotokana na ugonjwa huo 73 ni wale wasiopata chanjo.
Ummy amesema hayo jijini Dar es Salaam, baada ya kupokea chanjo nyingine dozi 800,000 aina ya Sinopham kutoka nchini China, Waziri Ummy, amesema takwimu za watu wanaopata chanjo bado haziridhishi na kati ya kundi lililo katika hatari kubwa ya ugonjwa huo ni watu wasiochanja.
Ametumia fursa hiyo kuthibitisha kuwa, hadi sasa hakuna taarifa ya mtu hata mmoja aliyeripotiwa kupata madhara kutokana na kupatiwa chanjo zaidi ya maudhi madogo madogo, hivyo aina zote za chanjo zilizoingia nchini ni salama na zimethibitika kuongeza kinga ya mwili na kupunguza makali ya ugonjwa huo.
Amemtaka Mganga Mkuu wa serikali na watendaji wake, kuhakikisha wanatoa taarifa mara kwa mara za ugonjwa huo na namna wasiochanja wanavyosababisha madhara.
NA MARIAM MZIWANDA