WATU watano wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam kujibu shtaka la unyang’anyi wa simu na Tsh. 2,000 kwa kutumia silaha aina ya panga.
Abubakari Gombo (28), Kennedy Deus (20), Musa Shabani (25),Ramadhani Abdallah (29) na Zuberi Issa(26) wamefikishwa Mahakamani hapo na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda, mbele ya Hakimu Mkazi, Sifa Jacob.
Mwaitenda alidai washtakiwa walitenda kosa hilo, Februari 8, mwaka huu, eneo la Kibamba Mdidimuo, Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam.
Washtakiwa hao wanadaiwa siku hiyo waliiba simu aina ya LG style4 yenye thamani ya sh.900,000 na sh. 2,000, mali ya George Gabriel.
Ilidaiwa kabla na baada ya kutenda kosa hilo, washtakiwa walimtishia kwa panga Gabriel ili kujipatia mali hizo.
Washtakiwa walikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu Jacob aliwaeleza washtakiwa shtaka lao halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo watarudishwa rumande na shauri liliahirishwa hadi Septemba 27, mwaka huu.
Na MEKI KIPALILO (TUDARCo) NA HAWA NGADALA