MKAZI wa Mbagala Kuu, Dar es Salaam, George Mwakang’ata (38) na wenzake wawili, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na shitaka la kusafirisha kilogramu 1.2 za dawa za kulevya aina Heroin.
Washitakiwa wengine katika kesi hiyo ni Andrew Paul wa Kurasini (34) na Said Mgoha, mkazi wa Mtoni Kijichi, Wilaya ya Temeke, Mkoani Dar es Salaam.
Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rita Tarimo, Wakili wa serikali Yusuf Aboud amedai, washtakiwa hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Juni 21, mwaka huu, eneo la Mivinjeni, Temeke Dar es Salaam.
Baada ya kusomewa shitaka lao, upande wa mashtaka umedai, upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kesi imeahirishwa hadi Julai 27, mwaka kwa huu, kwa ajili ya kutajwa.
Washitakiwa wote wamepelekwa mahabusu kwakuwa shitaka linalowakabili halina dhamana na hawakutakiwa kujibu lolote, kwakuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi husika.
Na Rehema Mohammed