WATU watatu wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kujibu shtaka la wizi wa simu kwa kutumia silaha aina ya kisu.
Festo Erinest (23), Mohamed Hemed (30) na William Anton (29), walisomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali, Debora Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi, Khadija Msongo.
Debora alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo, Mei 20, mwaka huu, eneo la Coco Beach, Wilaya ya Kinondoni, ambapo waliiba simu aina ya iPhone plus yenye thamani ya sh. 850,000.
Alidai kabla na baada ya kufanya wizi, walimtishia Leah Saruma kwa kisu ili kupata mali hiyo.
Washitakiwa hao walikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Washitakiwa walirudishwa mahabusu hadi Oktoba 25, mwaka huu, baada ya Hakimu kuwaeleza kuwa shtaka linalowakabili halina dhamana.
Wakati huo huo, Halid Abdallah, Fausta Yobu na Helena Donat walifikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, wakikabiliwa na shtaka la kuuza dawa za kulevya.
Abdallah (29), Fausta (39) na Helena (46), walifikishwa mahakamani hapo na kusomewa shtaka na Wakili wa Serikali, Benson Mwaitenda, mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Aaron Lyamuya.
Mwaitenda alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo, Agosti 30, mwaka huu, eneo la Mbezi, stendi ya mabasi ya mikoani Magufuli, ambapo walikutwa na dawa za kulevya aina ya bangi yenye uzito wa gramu 103.87.
Washitakiwa hao walikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu aliwaeleza washitakiwa hao kuwa shauri hilo linadhaminika kwa masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili ambao watatia saini dhamana ya sh. milioni moja.
Abdallah na Helena walitimiza masharti ya dhamana huku Fausta akirudishwa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti. Kesi iliahirishwa hadi Oktoba 20, mwaka huu.
Na HAWA NGADALA