WATOTO wawili wa familia moja wamefariki dunia, baada ya kukosa hewa ya kutosha chumbani katika nyumba waliyokuwa wakiishi iliyoko Kijiji cha Usubilo, Kata ya Ifucha, Halmashauri ya Manispaa Tabora.
Katika tukio hilo, pia baba mzazi wa watoto hao na mama yao na dada yao walijeruhiwa na wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa huo (Kitete) kwa matibabu zaidi, huku ikielezwa kwamba hali zao hadi sasa hazijaimarika vizuri.
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Richard Abwao, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwataja watoto waliofariki dunia ni Amani Athuman mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu na Zainabu Athumani wa mwaka mmoja.
Kamanda Abwao alisema tukio hilo lilitokea Februari 5, mwaka huu, saa 6.30 usiku, kijijini humo, huku chanzo kikitajwa ni moto uliokuwa umewashwa ndani ili kuwapa joto watoto hao kutokana na baridi kali kipindi hiki cha mvua.
Alieleza kuwa moshi wa moto huo ulisababisha watoto hao waliokuwa wamelala kukosa hewa ya kutosha kutokana na miundombinu duni ya kupitisha hewa katika nyumba hiyo.
Kamanda huyo alisema miili ya watoto hao ilifanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa ndugu ili kuendelea na utaratibu wa mazishi.
Aliwataja wahanga wengine katika tukio hilo ni baba mzazi wa watoto hao, Athuman Shaban (45) Mnyamwezi, mkulima, mkewe Magreth Joseph (34) Msukuma, mkulima na binti yao Neema Athumani (17) wote ni wakazi wa Ifucha.
Alibainisha kwamba majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa huo (Kitete) kwa ajili ya matibabu zaidi na hali zao hadi sasa hazijaimarika.
Kamanda huyo alitoa wito kwa wananchi kuangalia usalama wa watoto wao, hususan katika kipindi hiki ambapo mvua zinaendelea kunyesha kwa wingi katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo ili wasidhurike.
Na Allan Kitwe, Tabora