WATU 13 wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Wilaya ya Bukoba, kwa tuhuma za uhujumu uchumi na kuisababishia serikali hasara ya sh. bilioni mbili.
Washitakiwa hao walisomewa mashitaka ya kukutwa na vifaa vya kufungia umeme, vilivyoibiwa katika mradi wa kusambaza umeme vijijini wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), awamu ya tatu mzunguko wa kwanza vilivyoibiwa mwaka 2019.
Kwa mujibu wa hati ya mashitaka, waliofikishwa mahakamani hapo ni Vitus Yamola, Michael Nyambole, Mtemi Amosi, Geradi Mpelembwa, Dalton Amphrey, Jumanne Hamed, Brighton Kundi na Ombeni Zakayo.
Pia, wamo Japhar Protasi, Yasir Armi, Kharim Senga, Geofrey Kundi na Lotangamwaki Milanyi. Kati ya washitakiwa hao wapo wanunuzi wa vifaa, wasafirishaji na wauzaji.
Mbele ya Hakimu Andrew Kabuka, Wakili wa Serikali, Juma Mahona, aliwasomea washitakiwa mashitaka ya kuongoza genge la uhalifu na kuisababishia mamlaka husika hasara hiyo.
Mahona alidai vifaa hivyo viliibiwa wakati kampuni iliyokuwa imepewa kazi ya kujenga mradi huo ya Nakuroi Investiment, ikiendelea na kazi ya kufunga umeme vijijini.
Alidai vifaa hivyo viliibiwa maeneo ya Mkoa wa Kagera na kukutwa wilayani Karagwe.
Hakimu Kabuka aliagiza Afidhi Kalugira ambaye ni mdhamini wa mshitakiwa namba 11 kumleta mahakamani Januari 17, mwaka huu na kuonya endapo hatafanya hivyo sheria itachukua mkondo wake.
Kabuka alisema kesi hiyo itatajwa Januari 30, mwaka huu na washitakiwa wanne walirudishwa rumande baada ya kutokamilisha masharti ya dhamana na wengine wakiachiwa kwa dhamana.
Na Angela Sebastian, Bukob