WATU wanne wakiwamo waganga wawili wa jadi, wanashikiliwa na Polisi mkoani Tabora, kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya viungo vya binadamu zikiwemo sehemu za siri.
Kamanda wa Polisi, mkoani humo, ACP Richard Abwao, alithibitisha hayo Februari 15, 2022 na kusema kati ya watuhumiwa hao, wawili wanatuhumiwa kukata viungo hivyo na kwenda kiviuza kwa waganga hao wa kienyeji.
“Kati ya watuhumiwa wanne, wawili ni waganga wa kienyeji ambao hutumia viungo vya binadamu katika shughuli zao, na wawili wanahusika katika mauaji na kukata viungo hivyo kwa binadamu. Tunaendelea na mahojiano nao,” alisema.
Alifafanua katika mahojiano na mtuhumiwa mmoja ambaye ni mganga wa kienyeji, alikiri kupelekewa viungo mbalimbali vya binadamu na kuvinunua kwa makubaliano.
Kamanda huyo alibainisha watuhumiwa wengine walikiri kuhusika na mauaji yaliyotokea maeneo mbalimbali.
Akifafanua namna wanavyotekeleza mauaji hayo, ACP Abwao alisema baada ya kufanya mauaji hutumia kitu chenye ncha kali kuwachoma ili kupata damu wanayoikinga katika chupa.
Alieleza kuwa, baada ya kuikinga damu hiyo wanakwenda kuiuza kwa waganga wa kienyeji kwa sh. 600,000.
Aliongeza pamoja na damu hiyo, pia wanawauzia viungo vya mwili na kulipwa kulingana na makubaliano yao.
Hata hivyo, Kamanda alisema mmoja wa watuhumiwa hao aliwataja watu wengine anaoshirikiana nao katika utekelezaji wa mauaji hayo na kwamba uchunguzi unaendelea.
“Baada ya tukio la mauaji ya mwanafunzi wa Shule ya Msingi Tutuo, tulianza operesheni hii na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa wanne hadi sasa, lakini bado tunaendelea hadi tutakapofanikiwa kuuzima mtandao wa wahalifu,” alisema.
Kwa mujibu wa Kamanda huyo, operesheni ilianza Januari 21, mwaka huu.
Hivi karibuni, Kamanda huyo wa polisi alitoa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tukio la kuuawa mwanafunzi huyo wa shule ya Msingi Tutuo (14) mauaji ambayo yalitekelezwa na watu ambao hawakuwa wamefahamika.
Na JUMA ISSIHAKA