WATU takribani milioni tano wanatarajiwa kupatiwa kinga ya magonjwa ya mabusha na matende mkoani Dar es Salaam.
Kinga hiyo itatolewa Oktoba 24 hadi 29, mwaka huu na serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele (NTDCP).
Akizungumza Dar es Salaam, Ofisa wa Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Magonjwa Yaliyokuwa Hayapewi Kipaumbele wa Wizara hiyo, Oscar Kaitaba, amesema kinga hiyo itatolewa katika Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, Temeke na Kinondoni.
“Kinga tiba hii itahusisha vidonge vya Albendazole na Netican na wahusika ni watu wote kuanzia umri wa miaka mitano na kuendelea, isipokuwa mtu anayenyonyesha kabla ya kutimiza siku saba, wagonjwa mahututi na wajawazito,” amesema.
Amesisitiza utoaji wa kinga tiba hiyo, utafanyika katika maeneo yote muhimu ambavyo ni vituo vya mabasi, treni, vyuo, shule, maeneo ya vyombo vya ulinzi na usalama, ofisini, nyumba kwa nyumba, vituo vya afya na kutakuwa na vituo vinavyo hama hama.
“Vidonge hivi ni salama na ni muhimu kwa wanawake na wanaume, kwasababu mabusha na matende yanasababishwa na mbu, wanaosababisha minyoo ambayo ikiziba mahali katika mwili wa binadamu inasababisha matende au busha,” alisema.
Mganga na Mafitiki kutoka Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Bionadamu (NIMRI), Dk. Wilfred Mandara, alisema gharama ya kutibu matende na mabusha ni kubwa, hivyo ni muhimu watu kupata kinga.
Mratibu wa NTDCP, Mkoa wa Dar es Salaam, Alex Mkamba, alisema, utoaji wa kinga tiba za matende na mabusha unahusisha Ilala, Kinondoni na Temeke kwa kuwa Ubungo na Kigamboni zilishatokomeza maradhi hayo.
“Ugonjwa wa matende na mabusha ni wa fedheha kubwa, hivyo tunawasihi wananchi wapate vidonge hivi vya kinga ni bure kabisa,” alieleza.
Ofisa Programu wa NTDCP wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Chihiyo Mlaya, aliwataka waandishi wa habari kusaidia kuelimisha jamii kuhusu umuhimu ya kinga hiyo.
Na CHRISTOPHER LISSA