WAKAZI wawili wa Dar es Salaam wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kujibu tuhuma za mauaji ya mama na watoto wake wawili yaliyotokea Masaki.
Washitakiwa hao Shadraki Kapanga (34) na Edward Tawala (52), walifikishwa Mahakamani hapo na kusomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali, Daisy Makakala, mbele ya Hakimu Mkazi, Sifa Jacob.
Daisy alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo, Juni 9, mwaka huu, eneo la Masaki, Kinondoni, Dar es Salaam, ambapo waliwaua mama Emilly Mutaboyerwa na watoto wake Damita Mutaboyerwa na Daniela Mutaboyerwa.
Washitakiwa hawakutakiwa kujibu shitaka hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu aliwaeleza washitakiwa kwamba Mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo, hivyo watarudi mahabusu hadi shauri litakapopelekwa na kusikilizwa Mahakama Kuu.
Washitakiwa hao walirudishwa rumande hadi Julai 19, mwaka huu.
Wakati huo huo, mwanafunzi wa chuo aliyejulikana kwa jina la Catherine (20), alifikishwa Mahakamani hapo kujibu shitaka la kutoa mimba kwa vidonge.
Akimsomea shitaka hilo, Wakili wa Serikali, Hilda Katto, alidai mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Ester Mwakalinga, kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo, Mei 4, mwaka huu, eneo la Magomeni, ambapo alitoa mimba kwa kutumia vidonge.
Mshitakiwa huyo alikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu alimweleza mshitakiwa huyo kuwa shitaka linalomkabili linadhaminika na kumtoa masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili ambao watatia saini bondi ya dhamana ya sh. milioni mbili. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 3, mwaka huu.
SAUMA MWANSHULI (UoI) Na HAWA NGADALA