SERIKALI imesema watumishi 1,491 wa darasa la saba walioondolewa kazini kwa kutokuwa na elimu ya kidato cha nne na kushindwa kujiendeleza hadi Desemba mwaka jana, watalipwa stahiki zao.
Imesema hatua hiyo ni utekelezaji wa agizo la Rais Samia Suluhu Hassan, tayari Mei 21 mwaka huu, serikali imetoa waraka kwa waajiri kuhakiki madeni na stahiki za watumishi hao ili waweze kulipwa.
Kauli hiyo, imetolewa bungeni wakati Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, Deo Ndejembi, alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Mikumi (CCM), Dennis Londo.
Katika swali lake, Londo aliuliza ni watumishi wangapi wamerejeshwa kazini baada ya kuondolewa kimakosa wakati wa zoezi la uhakiki wa vyeti feki na wafanyakazi hewa na watumishi wangapi waliorejeshwa kazini, wamelipwa stahiki zao kama mishahara ambayo hawakupata kutokana na kuondolewa kimakosa.
Akijibu swali hilo, Ndejembi alisema serikali Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, imewarejesha kazini na kuendelea kuwalipa mishahara watumishi 4,380 walioondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara kimakosa wakati wa uhakiki wa vyeti vya elimu na watumishi hewa.
Alisema idadi hiyo inajumuisha Watendaji wa Kata, Watendaji wa Vijiji na Watendaji wa Mitaa wapatao 3,114.
“Pamoja na kuwarejesha watumishi tajwa, serikali pia ilitoa msamaha wa kuwarejesha kazini watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya kidato cha nne na baadaye wakajiendeleza na kupata sifa tajwa hadi kufikia Disemba, 2020 ambao hawakudanganya katika taarifa zao kuwa wana elimu ya kidato cha nne au kubainika kughushi vyeti.
“Pia, mnamo Mei saba, 2021 serikali kupitia ofisi yangu ilitoa maelekezo na utaratibu kwa waajiri kuhusu namna ya kushughulikia hatima za ajira za watumishi walioondolewa kazini kwa kukosa sifa ya elimu ya kidato cha nne pamoja na malipo ya stahili zao,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa: “Napenda kuwakumbusha waajiri wote kukamilisha utekelezaji wa maelekezo hayo kwa haraka na kwa usahihi ili watumishi husika waweze kupata haki zao mapema.”
Alisisitiza kwamba msamaha uliotolewa unawahusu watumishi ambao waliajiriwa baada ya Mei mbili mwaka 2004 bila sifa ya elimu ya kidato cha nne, lakini baadaye wakajipatia sifa za kuajiriwa na hauwahusu watumishi waliobainika kuwa na vyeti vya kughushi au waliotoa taarifa za uongo katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi.
Naibu waziri huyo alisema utaratibu wa kushughulikia watumishi waliobainika kughushi vyeti ulishatolewa awali na serikali na watumishi wote waliobainika kughushi vyeti hawastahili kurudishwa kazini wala kupata malipo yoyote.
“Serikali imelipa madai ya mishahara ya jumla ya sh. bilioni 2.6 kwa watumishi 1,643 waliorejeshwa kazini baada ya kuondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara kimakosa. Uhakiki wa madai yaliyobaki unaendelea na yataendelea kulipwa kwa kadri yanavyohakikiwa,” alieleza.
Baada ya majibu hayo, Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma, alisimama kuuliza swali la nyongeza ambapo katika swali lake alisema licha ya uamuzi huo wa serikali bado wapo waliokuwa watumishi walioondolewa kwa kukosa cheti cha kidato cha nne ambao hawajalipwa stahiki zao au kupokelewa na waajiri wao.
Aliiomba serikali iwapatie wabunge nakala ya wakara huo ili waitumie katika kuwatetea watumishi hao walioondolewa kazini.
Akijibu swali hilo, Ndejembi alisema watumishi ambao hadi sasa hawajajiendeleza kielimu 1491 kati ya watumishi 4380 waliokuwa na kiwango cha elimu ya darasa la saba.
Alisisitiza waajiri waendelee kuhakiki madeni na stahiki za watumishi hao 1,491 ili waweze kulipwa stahiki zao.
Na MUSSA YUSUPH, DODOMA