WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameziagiza mamlaka husika kuchukua hatua kali za kisheria kwa watakaobainika kuwanyanyapaa na kuwabagua watu wanaoishi na virusi vya Ukimwi (WAVIU) kwa kuwa vitendo, kauli au mitazamo hiyo havikubaliki.
“Kumekuwa na madai kuwa watumishi wa afya wana tabia za unyanyapaa na kuvujisha siri za WAVIU wanapotoa huduma katika vituo vyetu vya tiba na matunzo kwa WAVIU. Vitendo na tabia hizi ziripotiwe mara moja pindi vitakapotokea.”
Alitoa agizo hilo wakati alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani ambayo kitaifa yamefanyika Uwanja wa Ruanda-Nzovwe mkoani Mbeya. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo inasema “Zingatia Usawa. Tokomeza Ukimwi. Tokomeza Magonjwa ya Mlipuko.”
Majaliwa alisema nchi ina sheria ya Ukimwi ambayo imefanyiwa marekebisho kadhaa ili kuhakikisha huduma za VVU na Ukimwi zinamfikia kila mlengwa. “Ninaelewa kuwa unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU bado ni changamoto kubwa katika jamii zetu.”
“Hii inatukwaza na kurudisha nyuma juhudi za mwitikio wa mapambano dhidi ya Ukimwi nchini. Mfano baadhi ya watu wanaoishi na VVU wanaona aibu kutumia huduma za VVU na Ukimwi zilizopo kwa sababu ya unyanyapaa na ubaguzi, hasa katika maeneo ya vijijini.”
Akizungumzia kuhusu kaulimbiu ya maadhimisho hayo, Majaliwa alisema kaulimbiu hiyo ni thabiti kwa sababu inatoa mwelekeo bora wa jinsi ya kuondoa changamoto zilizopo ili kupata matokeo bora zaidi kwa kila wanachofanya katika miradi na afua za udhibiti Ukimwi nchini usawa lazima uzingatiwe.
“Usawa unahitajika kwenye mahitaji ya msingi ya makundi mbalimbali Ukimwi hauchagui umri, jinsi wala rika. Hivyo kaulimbiu hii inatukumbusha wajibu wetu wa kuzingatia utoaji wa huduma kwa makundi yote ambayo ni pamoja na watoto, vijana, wanawake, wasichana, wanaume, wazee, watu wenye ulemavu na makundi yaliyo katika mazingira hatarishi zaidi.”
Hivyo, Waziri Mkuu alisema ili kutekeleza kwa vitendo kaulimbiu hiyo uwekezaji unatakiwa uzingatie mahitaji halisi kwa kila kundi, mazingira halisi na uhatarishi uliopo. “Licha ya hayo haki za binadamu pia zizingatiwe ili huduma zote zinazohusu masuala ya VVU na Ukimwi zitolewe kwa usawa unaohitajika.”
Kadhakika, Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wadau wote kuwa serikali inaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kuhakikisha uendelevu wa afua za VVU na Ukimwi nchini kwa kuweka mikakati ya kukusanya rasilimali za ndani.
Kwa upande wake, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, alisema huduma za ARV kwa watu wanaoishi na VVU zinaendelea kuimarishwa kwa kuhakikisha wanaogundulika wanapaswa kuanza kutumia ARV mapema na kuzingatia usahihi wa huduma hizi.
Alisema katika kudhibiti kuenea kwa maambukizo mapya ya VVU, serikali kwa kushirikiana na wadau wake inaendelea kutekeleza mkakati wa nne wa kudhibiti Ukimwi kwa kushirikisha sekta zote nchini. Mkakati huo wa mwaka 2018/2019 hadi 2022/2023 umelenga kupunguza maambukizi mapya ya VVU na vifo vinavyohusiana na UKIMWI.
Naye, Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya UKIMWI (NACOPHA), Leticia Maurice alimpongeza Rais Samia kwa maono na jitihada zake za kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali nchini ikiwemo ya afya.
Na MWANDISHI WETU