WAKAZI wawili wa Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni, kujibu shtaka unyang’anyi wa kutumia silaha.
Washitakiwa hao ni Hamis Said (22) na Issa Twaha(22), ambao walisomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali, Veronica Mtafya, mbele ya Hakimu Mkazi, Sifa Jacob.
Veronica alidai washitakiwa hao walitenda kosa hilo, Desemba 25, mwaka jana, eneo la Magomeni, Wilaya ya Kinondoni.
Alidai washitakiwa waliiba simu aina ya Tecno yenye thamani ya sh.80,000, fedha taslimu sh. 150,000, mali ya Fetaheri Sadick Elly.
Ilidaiwa kabla na baada ya kufanya wizi huo, walimtishia kwa panga Elly ili kupata mali hiyo.
Washitakiwa walikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba Mahakama kupanga tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Hakimu aliwaeleza washitakiwa kwamba shtaka linalowakabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria, hivyo walirudishwa mahabusu hadi Novemba mosi, mwaka huu, kesi itakapopelekwa kwa usikilizwaji wa awali.
Wakati huo huo, watu wawili walipandishwa kizimbani mahakamani hapo wakikabiliwa na shtaka la wizi wa gari.
Washitakiwa hao Yusufu Rajabu na Nasoro Santo, walisomewa shtaka hilo na Wakili wa Serikali, Debora Mushi, mbele ya Hakimu Mkazi, Khadija Msongo.
Debora alidai washitakiwa walitenda kosa hilo, Septemba 20, mwaka huu, eneo la Oysterbay-viwanja vya mbwa na farasi Wilaya ya Kinondoni, ambapo waliiba gari lenye namba za usajili T 299 DTM aina ya Subaru Impreza lenye thamani ya sh. milioni 12.5, mali ya Rogasian Mella.
Washitakiwa walikana kutenda kosa hilo, ambapo upande wa Jamhuri ulidai upelelezi umekamilika na kuomba kupangiwa tarehe ya usikilizwaji wa awali.
Washitakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa wadhamini wawili kila mmoja na kutia saini fungu la dhamana la sh. milioni saba na shauri liliahirishwa hadi Novemba 3, mwaka huu.
Na HAWA NGADALA