WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk. Dorothy Gwajiama, amewataka wanawake wasikalie kulalamika, bali wachukue hatua dhidi ya vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa.
Pia, watumie majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi ikiwa ni pamoja na kudai haki yao ya mikopo inayopaswa kutolewa na kila halmashauri nchini na asilimia zake katika mabano vijana (asilimia nne), wanawake (asilimia nne) na watu wenye ulamavu (asilimia mbili).
Dk. Dorothy aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa Kongamano la Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, ambalo kimkoa lilifanyika katika uwanja wa Nyamagana mkoani Mwanza.
“Kuna kamati za ulinzi wa mwanamke toka kila ngazi ya mtaa, kijiji, kata hadi wilaya, au hazifanyi kazi.
“Zitumieni kupaza sauti dhidi ya vitendo vya unyanyasaji na ukatili mnaofanyiwa na mchukue hatua, badala ya kukaa kulalamika tu kuwa mnanyanyaswa, serikali imetengeneza miongozo na wanawake mmeingizwa katika kamati hizo,” alisema.
Aliwataka wanawake wasibweteke na kuishia kusema wamepata Rais mwanamke Rais Samia Suluhu Hassan au kuishi kumshukuru Rais kuwapa wizara, popote walipo wasilale, wawe majasiri wa kudai haki zao na wachapekazi, vinginevyo watabaki kulalamika.
Dk .Dorothy alisema wanawake wanatakiwa kuinuka kitakwimu kipindi kijacho cha uongozi, hivyo pamoja na kutakiwa kujitokeza kwa wingi wakati wa Sensa ya Watu na Makazi wahesabiwe ili wamtendee haki Rais Samia, mwaka 2025 wajitokeze kuwania uongozi katika ngazi mbalimbali.
Waziri huyo aliitaka jamii kutofumbia macho masuala ya ukatili na unyanyasaji kwa sababu, hakuna nafasi au muda unaotengwa kuzungumzia hayo yanayotokea katika jamii na kuwataka wanaume wasilalamike kuwa wameachwa katika haki.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Robert Gabriel, aliwataka wanawake wasiwatenge wanaume katika familia zao kwa kupiga maombi, bali watumie akili na maarifa waliyopewa na Mungu.
“Mwanaume anahitaji ulinzi wako mwanamke, hivyo siyo kila jambo unakimbilia polisi au kwa wakwe, jitambueni na kuchanganya maarifa katika malezi, msiingie katika mapenzi bila maarifa, akili na kumcha Mungu, watiini na kuwathamini waume zenu,” alisema.
Naye, Mkurugenzi wa shirika lisilokuwa la kiserikali la Kivulini linalopigania haki na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini, Yassin Ally, alisema wanampongeza Rais Samia kwa kuipaisha Tanzania kiuchumi, biashara, uwekezaji, siasa, elimu na jinsia.
“Rais aliyoyafanya kwa mwaka mmoja ni makubwa na mengi zaidi ya kipindi hicho, kinamama ni msingi wa takwimu, naomba mjitokeze kwa wingi katika sensa ya watu na makazi itakayofanyika Agosti, mwaka huu,” alisema.
NA PETER KATULANDA, Mwanza