WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dk.Dorothy Gwajima, amewaagiza watendaji wa wizara hiyo kuhakikisha wanazingatia jukumu lao la msingi la kutengeneza miongozo, sera na ufuatiliaji ili ubaguzi wa kijinsia usionekane na kuchukua nafasi katika jamii.
Pia amesema Sera mbalimbali ikiwemo ya Maendeleo ya Jamii zimepitwa na wakati hivyo wako katika mkakati wa kuwakutanisha wadau ili kuzifanyia upya mapitio kwa lengo la kuzifanyia marekebisho.
Dk.Dorothy ametoa maelekezo hayo jiji Dodoma wakati akizungumza katika kikao cha kwanza cha menejimenti kilichokuwa na lengo la kujenga uelewa wa pamoja na kufanya uchambuzi wa walipotoka, walipo na wanapotaka kuelekea.
Amesema wizara hiyo inajukumu la kuhakikisha inazingatia jukumu lao la msingi la kutengeneza miongozo, sera na ufuatiliaji ili ubaguzi wa kijinsia usionekane na kuchukua nafasi katika jamii hivyo watakeleze kikamilifu jukumu hilo.
Waziri huyo akizungumzia lengo la kuwakutanisha wadau ni kuona namna ya kufanya marekebisho kwenye sera mbalimbali ili ziandane na wakati wa sasa wa sayansi na Teknolojia.
“Sera nyingi zimepitwa na wakati na zimekuwa za siku nyingi ambapo maendeleo ya jamii wana sera imepitwa na wakati na ina miaka 25 sasa tangu itungwe,”amesisitiza Dk.Dorothy.
Ametolea mfano moja wapo ambayo imepitwa na wakati kuwa ni sera ya wanawake ambayo inazaidi ya miaka 25 na sera ya wazee na watoto na kwamba zote zinahitaji kufanyia marekebisho kwa kushirikiana na wadau ili kuleta matokeo chanya.
“Kazi hiyo ya mapitio ya sera inapaswa kufanywa haraka ili kupata sera mpya jambo ambalo ni matamanio ya Rais Samia Suluhu Hassan,”amesema Waziri huyo.
Amesema katika kuweka mifumo katika maendeleo ya jamii inapaswa kwenda sambamba na kuangalia usawa wa kijinsia kwani kila mmoja ana haki sawa na anaweza kutekeleza majukumu au kufanya Mambo ya msingi kama mwingine.
“Yapo mambo ya kijinsi kama kubeba mimba,kujifungua haya tunajua mwanaume hawezi kuyafanya hivyo basi kwenye majukumu hayo aheshimiwe ili atupatie mtoto mzuri,na akimaliza jukumu hilo la kibaiolojia akaja kwenye majukumu mengine ya pamoja yasitazamwe kwa ubaguzi wa kijinsia,”amesema Dk. Dorothy
Amesema wizara hiyo inaowajibu mkubwa wa kuhakikisha inakuwa kichocheo cha maendeleo kwa jamii na kila mtu ananufaika na fursa zilizopo nchini Ili jamii na kwamba jamii inahitaji kuishi kwa amani na utulivu.
Na Happiness Mtweve,Dodoma