WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Jenister Mhagama, ameitaka mifuko ya hifadhi ya jamii kwa watumishi wa umma na binafsi NSSF na PSSSF, kuhakikisha wanaweka mifumo inayoonana na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA),Mamlaka ya Mapato (TRA) na wafanyakazi waone michango yao kwa kutumia mifumo ya kielektoniki.
Amesema utendaji wa mifuko hiyo umetoa ahueni kwa Watanzania, hivyo watendaji wahakikishe wanaweka mifumo stahiki inayosomana na mifumo mingine ya mamlaka zingine huku waajiri wakitakiwa kujisajili kwa hiyari kwa mifumo hiyo.
Waziri Jenista ametoa kauli hiyo katika Maonyesho ya 45 ya Biashara ya Kimataifa (Sabasaba), ambapo ametembelea mabanda ya taasisi mbalimbali zilizo chini ya wizara yake, ambazo zimeshiriki maonyesho hayo kwa mwaka huu.
Jenista amesema, pamoja na agizo hilo,Rais Samia Suluhu Hassan, ameonyesha ukomavu, ujasiri, uzalendo wa uongozi bora katika siku zaidi ya 100 madarakani hususani kwenye usimamizi wa mifuko ya hifadhi ya jamii.
Amesema utendaji wa Rais Samia, umekuwa na uthubutu wa kulipa malimbikizi ya madai ya muda mrefu ya zaidi ya sh. bilioni 300 za mifuko hiyo kwa serikali.
Waziri Jenista amesema hadi sasa, tayari sh. bilioni 100, zimetolewa na maelekezo yake kwa watendaji ni kuhakikisha deni hilo linalipwa haraka, ili wastaafu wapate haki zao kwa wakati.
“Utekelezaji wa mambo ya sekta ya jamii ni matakwa ya Kikatiba Ibara ya 11, wastaafu wengi waliokuwa watumishi wa umma walikuwa hawapati mafao yao kutokana na deni la serikali, ameonyesha ujasiri na ameagiza kufanyika tathmini ili kuwa na mifumo endelevu isiyosumbua wastaafu,” amesema.
Na Mariam Mziwanda
PICHA: WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, akizungumza na Joel Charles, aliyefika kupata huduma katika banda la Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), wakati wa Maonyesho ya Biashara ya Kimataifa, barabara ya Kilwa, Dar es Salaam. (Picha na Jumanne Gude).