WAZIRI wa Afya, Ustawi wa Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, amesema amethibitika kuwa na maambukizi ya maradhi ya Uviko- 19, amejitenga kwa muda wa wiki moja.
Amesema hii ni mara yake ya kwanza kupata maradhi hayo na kutoa wito kwa Wazanzibar kuendelea na jitihada za kujikinga na Uviko-19.
Mazrui aliyasema hayo alipozungumza na UHURU kwa njia ya simu na kufafanua kuwa aligundulika kuwa na maradhi hayo Desemba 24, mwaka huu (Ijumaa) na kwa sasa amejifungia nyumbani kwake kwa muda wa wiki moja.
“Usiku wa kuamkia Alhamisi nilianza kujisikia homa kali na kuharisha, ndipo nilioamua kwenda hospitali siku ya Ijumaa na waliponipima nilikutwa na Uviko-19,” alisema.
Aliongeza kuwa baada ya kukutwa na hali hiyo, aliamua kujitenga, ambapo kwa sasa afya yake inaendelea kuimarika.
“Nimejifungia chumbani na mtu akija, basi naongelea dirishani kwa kuepusha kuwaambukiza wengine maradhi haya,” alieleza Marzui.
Aliwataka wananchi wa Zanzibar kuendelea na jitihada za kulinda na Uviko-19, kwa kuwa bado ipo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Waziri huyo aliwasihi wananchi kuchukua tahadhari zote katika kujilinda na ugonjwa huo huku akiwakumbusha suala zima la kuchanja.
Kwa mujibu wa Mazrui, ugonjwa huo umepungua kasi kwake kutokana na kupata chanjo.
“Binafsi yangu mafua yaliniathiri siku moja tu, ule usiku wa Alhamis na kukohoa siku ya pili yake, lakini haikuwa na kasi sana, hiyo ni kwasababu nilichanja,” alisema.
Aliendelea kuwasisitiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari kwa kupata chanjo na kuvaa barakoa na kunawa mikono kwa sabuni na vitakasa mikono na kuepiuka mikusanyiko isiyo ya lazima.
“Maradhi haya bado yapo na watu wengi sana wameathirika na wengine hawaendi hospitali wanabaki nyumbani. Hivyo, niwaambie tu wasibakie nyumbani waende kupima na kama watakutwa na Uviko-19 basi washughulikiwe,” alisistiza.
Alisema wananchi wengi wanapoona dalili za mafua na vifua hawaendi hospitali, badala yake wanajifukiza tu, jambo ambalo siyo zuri kwa afya zao.
HANIFA RAMADHANI NA EMMANUEL MOHAMMED, ZANZIBAR