WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameeleza kusikitishwa na tabia ya baadhi ya vigogo kukaidi utaratibu wa usalama ukiwemo ukaguzi wa kawaida katika viwanja vya ndege nchini.
Profesa Mbarawa pia ameziagiza taasisi zote zinazohusika na huduma za usafiri wa anga, kuwa na mikakati endelevu yenye lengo la kuboresha hali ya usalama wa usafiri wa anga katika viwanja hivyo.
Alizitaja taasisi hizo ni Mamlaka ya Usafiri wa Anga, kampuni na shirika la ndege nchini, mawakala wa huduma za ndege katika viwanja vya ndege, watoa huduma za vyakula, bidhaa na huduma nyingine muhimu.
Waziri aliyasema hayo jijini Dar es Salaam, katika ofisi za makao makuu ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Nchini (TCAA), wakati akizindua mwaka wa utamaduni wa kiusalama wa usafiri wa anga, ambao unatambuliwa duniani kote kupitia mwamvuli wa Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (ICAO).
“Ninaongea kwa masikitiko makubwa, nina taarifa za uwepo wa baadhi ya watumishi wakiwemo wakuu kwenye baadhi ya taasisi zinazofanya kazi hapa viwanja vya ndege, wakikaidi kutekeleza matakwa ya kiusalama au kudharau taratibu za kiukaguzi, hili jambo sio sahihi.
“Mimi mwenyewe Waziri mwenye dhamana ya hii sekta nikipita mle mote nahakikisha ninakaguliwa, ninavua viatu, ninavua mkanda na kufanya kila ninachotakiwa kufanya kwa mujibu wa sheria.
“…sasa ninawashangaa kabisa wakuu wa taasisi wanaopita na wanasema ‘mimi ni mkuu wa taasisi wa kiwanja cha ndege hiki, nisikaguliwe’ hili si sahihi, usalama wa viwanja hivi upo mikononi mwetu, kila mmoja atimize wajibu,” alisema.
Waziri huyo alisema kuhusu mikakati ya kitaasisi, inapaswa viongozi wawe mstari wa mbele kuongoza kampeni hiyo kwa vitendo, ili kuashiria kuwa usalama wa katika sekta ya anga ni kipaumbele, kuweka mazingira rafiki ya kuhamasisha utekelezaji wa majukumu ya usalama, kutoa mafunzo na kuboresha vitendea kazi na miundombinu.
Mbarawa alisema usalama katika usafiri wa anga ni mazingira ambayo hayajitokezi bila ushirikiano wa wadau wote wa sekta hiyo, hivyo mbinu za kuhakikisha usalama zinatakiwa kuwa endelevu na shirikishi ili ziwe na tija.
“Kukosekana usalama wa sekta, kumesababisha kupotea kwa maisha ya wasafiri na wasio wasafiri, upotevu wa mali, uharibifu wa miundombinu na kurotoza kwa shughuli za utalii na biashara duniani,” alisema.
Alisema tukio hilo maarufu kwa jina 9/11 litaendelea kuwa alama ya umuhimu wa kujali usalama wa usafiri wa anga, kazi ambayo inafanywa vizuri na ICAO kwa kushirikiana na nchi zingine wanachama ikiwemo Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Hamza Johari, alisema Tanzania imekuwa nchi ya tatu Afrika, kuadhimisha maelekezo hayo ya kidunia juu ya usalama wa usafiri wa anga.
Alisema, awali ICAO ilikuwa na viambatisho 16 vya kusimamia sekta ya usafiri wa anga, lakini kutokana na tukio la kigaidi la mwaka 2001 nchini Marekani, ambalo ndege zilitumiwa kama silaha, shirika hilo liliongeza viambatisho hivyo na kufikia 17.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu huyo wa TCAA, kwa upande wa Afrika hadi kufiki jana, nchi nne Tanzania, Ethiopia, Misri na Ghana ndizo zimetekeleza maagizo ya kuzindua mwaka wa utamaduni wa usalama wa usafiri wa anga.
Na WILLIAM SHECHAMBO