WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, ameahidi kuunda timu ya uchunguzi ili kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha inayotumika katika ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Arusha.
Profesa Mbarawa ameyasema hayo, baada ya kukagua upanuzi na ukarabati wa miundombinu ya maegesho ya ndege, magari na njia ya kuruka na kutua ndege katika uwanja huo.
“Nimekagua kazi ni nzuri, hongereni, ila nitaleta timu hapa iniambie hizi gharama za ujenzi mnazozitaja kama zinaendana na thamani ya fedha,” alisema Profesa Mbarawa.
Waziri huyo aliwataka wafanyakazi wa uwanja huo kufahamu umuhimu wao katika kutoa huduma bora kwa watalii na abiria wengine, ili kuvutia watu wengi kutumia miundombinu hiyo hatua itakayoongeza mapato.
Alisema uwanja huo ni wa tatu kwa mapato na wa pili kwa miruko ya ndege na abiria katika biashara ya usafiri wa anga hapa nchini, ukitanguliwa na Dar es Salaam (JNIA) na Mwanza, hivyo serikali inautazama kikamilifu.
Kwa upande wake, kaimu meneja wa uwanja huo, Reston Mtafya, alisema watumishi wamejipanga vizuri kimaadili, nidhamu na ubunifu ili kuleta tija katika kazi zao.
“Tumejipanga kuhakikisha uwanja wetu unatumiwa na abiria wengi kwa kutoa huduma za viwango vya juu,” alisisitiza Mtafya.
Katika hatua nyingine, Waziri Mbarawa alikagua karakana ya Wakala wa Ufundi na Umeme Nchini (TEMESA), mkoa wa Arusha na kuwataka kufanya kazi zinazopimika na kumpa ripoti za kazi kila mwezi.
Aliwataka kuhakikisha malalamiko ya watumiaji huduma za TEMESA yanafika mwisho kwa kutoa huduma za kisasa, kibingwa na za haraka katika fani ya utengenezaji wa magari, mitambo na umeme.
“Kila mwezi nataka ripoti ionyeshe mmezalisha kiasi gani cha fedha, mmekusanya shilingi ngapi na mmetoa huduma kwa kiwango gani ili tuwapime na watakaoshindwa watupishe,” alisisitiza Profesa Mbarawa.
Pia alizungumzia umuhimu wa TEMESA kufanya majukumu yake ya msingi katika kutoa huduma na kuwatumia wahitimu wa VETA na Vyuo vya Ufundi, kufanya mazoezi ili kuwajengea uwezo wakati wanatafuta ajira.
Profesa Mbarawa yuko katika ziara ya siku tatu mkoani Arusha kukagua miradi ya maendeleo ya taasisi zilizo chini ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.
Na MWANDISHI WETU