WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Madini, kuhakikisha shughuli za uuzwaji na uzalishaji wa madini ya Tanzanite, zinafanyika Mererani ili kutunza na kuimarisha ulinzi wa madini hayo nchini.
Amesema kuruhusu Tanzanite kuchakatwa nje ya Mererani kunaweza kutoa mwanya wa kutoroshwa madini hayo nje ya nchi na kusababisha nchi nyingine kujivunia hali ya kuwa yanapatikana nchini pekee.
Akizungumza akiwa Simanjiro mkoani Manyara, baada ya kuzindua kituo cha madini ya Tanzanite, Waziri Mkuu Majaliwa alisema serikali imeimarisha ulinzi na kutoa ardhi, hivyo ni lazima shughuli zote ziishie katika eneo hilo.
“Nakuagiza Katibu Mkuu, madini haya ‘process’ (hatua) zote za biashara ya Tanzanite ziishie Mererani, lengo la serikali ni kuyafanya madini ya Tanzanite yanatambulika duniani kote,” alisema.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa, aliwaagiza wafanyabiashara wa Tanzanite hadi kufikia Oktoba 15, mwaka huu wahakikishe ofisi na viwanda vyao vya kuchakata madini hayo vinahamishiwa Mererani.
“Ninatoa miezi mitatu, kuanzia Julai 15, mwaka huu hadi Oktoba 15 mwaka huu, wafanyabiashara wote wa madini ya Tanzanite wawe wamehamishia ofisi zao na viwanda vya kuchakata Tanzanite hapa Mererani na baada ya muda huo tutatumia utaratibu maalumu kwa watakaokidi agizo hili,” aliagiza.
KATIBU MKUU MADINI
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Profesa Simon Msanjila, alisema kituo hicho kimegharimu sh. bilioni 1.4 na kimejengwa kwa ufanisi mkubwa ili kutoa huduma bora kwa wafanyabiashara. Aidha, Profesa Msanjila alisema udhibiti wa madini ya Tanzanite Mererani umeimarika kutokana na ukuta uliowekwa, kwa sababu umeboresha mazingira kwa wafanyabiashara hususan usiku.
“Mafanikio ya Mererani ni ushahidi tosha wa mafanikio katika sekta ya madini na kuchangia mapato ya serikali kupitia sekta ya madini,” alisema.
Aidha, Msanjila alisema ujenzi wa ukuta wa Mererani umesaidia kuongeza mapato kwa serikali ambapo katika kipindi cha mwaka 2018 zaidi ya kilo 781,204 za Tanzanite zimezalishwa zikiwa na thamani ya sh. bilioni 20 na kuiwezesha serikali kukusanya sh. bilioni 1.437.
WAZIRI WA ULINZI
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias Kwandikwa, alisema watashirikiana na Wizara ya Madini katika kutekeleza maagizo yote yanayotolewa na serikali.
Kwandikwa alisema Jeshi la Polisi lipo eneo hilo ili kuhakikisha Mererani inakuwa salama na shughuli zote zinafanyika vizuri pamoja na kutatua changamoto zilizopo. “Tutaendelea kusimamia taasisi zetu ili huduma hii muhimu ifanyike na mambo muhimu yaendelee,” alisema.
Kwa upande wake Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka, alisema kituo hicho kitakuwa chachu ya kuwasaidia vijana kifikra na kuondokana na changamoto ya ajira. Ole Sendeka alisema wadau wa madini wanatakiwa kukaa pamoja kuona namna gani wananufaika na madini hayo.
James Laizer ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara wa madini, aliomba serikali kuboresha miundombinu ya barabara katika mkoa huo, ili kuwasaidia kufanya shughuli zao ipasavyo.
Pia, aliiomba serikali kurejesha muda wa ufanyaji kazi katika eneo hilo kuwa saa 24 kama ilivyokuwa ikifanyika awali kwa kuwa uzalishaji wa madini umeongezeka.
LILIAN JOEL (Mererani) Na IRENE MWASOMOLA (Dar)
PICHA:WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa akifunua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Kituo cha Tanzanite-Magufuli kilichopo Mirerani Mkoani Manyara, Julai 7, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)